Gor Mahia kutafuta mkufunzi mpya iwapo Steven Polack atakosa kurejea
Na CHRIS ADUNGO GOR Mahia wametishia sasa kuajiri kocha mpya iwapo , mkufunzi Steven Polack hatarejea humu nchini kufikia mwisho wa wiki hii; yaani Oktoba 4, 2020. Polack aliondoka humu nchini mnamo Agosti na kuelekea Finland kwa likizo ya siku 10, lakini hajarejea hadi kufikia sasa jinsi ilivyotarajiwa. Licha ya kutorejelewa kwa shughuli za mchezo wa soka humu nchini, Gor Mahia ambao ni mabingwa mara 19 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), walianza kujifua upya kwa minajili ya kampeni za msimu ujao wa 2020-21 wiki mbili zilizopita chini ya kocha msaidizi Patrick Odhiambo. Mbali na kutetea ufalme wao wa Ligi Kuu msimu ujao, Gor Mahia pia wanalenga kupiga hatua zaidi kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League). Mhazini wa Gor Mahia, Dolfina Odhiambo amefichua mpango wa kuanza kupekuapekua wasifu-kazi wa baadhi ya wakufunzi waliowahi kutuma maombi ya kutaka kupokezwa mikoba ya Gor Mahia hapo awali. “Tumewahi kushuhudia visa ambapo wakufunzi wa Gor Mahia wanatumia visingizio vya kuenda makwao kwa likizo kisha wakakosa kabisa kurejea. Gor Mahia wamepania kuchukua tahadhari,” akatanguliza Odhiambo. “Tunatarajia Polack arejee kufikia mwisho wa wiki hii. Alitazamiwa kuwa amefika mapema zaidi ila tunaelewa kwamba kanuni za kudhibiti msambao wa corona zilimtia kwenye karantini kwa siku 14 alipowasili Finland,” akasema Odhiambo. “Iwapo hatakuwa amerejea kufikia mwisho wa wiki hii, basi tutalazimika kuingia sokoni kusaka kocha mpya. Tuna barua nyingi za maombi ya kazi ambazo tunaweza kutumia kupata kocha mpya kizibo cha Polack,” akasema. Klabu zinazotarajiwa kushiriki gozi la Ligi Kuu ya FKFPL msimu ujao wa 2020-21 tayari zimepokezwa seti ya kwanza ya mipira kutoka kwa jumla ya mipira 1,600 ya kwanza iliyopokelewa na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) mwanzoni mwa Agosti 2020. Kila kikosi kinachoshiriki kipute cha FKFPL, Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL) na Ligi Kuu ya Wanawake (KWPL) kinatarajiwa kupokea jumla ya mipira 20 huku kila klabu inayoshiriki soka ya madaraja ya chini kwa upande wa wanaume na wanawake ikipokea mipira 10. |