• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:07 PM
Gor Mahia yaajiri kocha Roberto Oliveira kuwa mrithi wa Polack

Gor Mahia yaajiri kocha Roberto Oliveira kuwa mrithi wa Polack

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA mara 19 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), Gor Mahia, wamejinasia huduma za kocha mpya, Roberto Oliveira.

Oliveira ambaye ni raia wa Brazil anajaza nafasi ya Mwingereza Steven Polack aliyejiuzulu usiku wa Oktoba 8, 2020, akiwa likizoni Finland.

Mwenyekiti wa Gor Mahia, Ambrose Rachier alithibitisha kuajiriwa kwa Oliveira saa 24 baada ya miamba hao kuagana na Polack aliyeaminiwa kuwa mrithi wa Mturuki Hassan Oktay mnamo Agosti 2018.

“Tuna furaha kutangaza ujio wa kocha mpya Roberto Oliveira ambaye ni raia wa Brazil. Anajivunia tajriba pana ya ukufunzi katika vikosi mbalimbali vya Afrika. Kuja kwake kutatupigisha hatua zaidi katika soka ya humu nchini na mapambano ya Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League),” akasema Rachier.

Oliveira ambaye anajivunia tajriba ya miaka 25 ya ukufunzi, amewahi pia kutia makali kikosi cha Rayon Sports ya Rwanda.

Amewahi pia kudhibiti mikoba ya timu mbalimbali za taifa barani Afrika, klabu za Uarabuni na vikosi vya Ligi Kuu ya Brazil.

Oliveira amewahi kuongoza Rayon kuvaana na Gor Mahia kwenye mashindano ya CAF miaka mitatu iliyopita.

“Baada ya kuondoka Rayon, nilipata ofa tatu za kurejea Afrika kudhibiti mikoba ya vikosi vya haiba kubwa. Nilipuuza ofa hizo zote hadi nilipopokea hii ya Gor Mahia,” akatanguliza Oliveira.

“Ilikuwa rahisi kuikubali ofa ya Gor Mahia kwa sababu ni kikosi ninachokifahamu vyema na nimewahi kuona wachezaji wake wakisakata boli dhidi ya klabu ya Rayon niliyokuwa nikiinoa. Nilivutiwa na mtindo wao wa mchezo na wamekuwa na historia ya kuridhisha katika soka ya Kenya.”

“Gor Mahia wanajivunia idadi kubwa ya mashabiki nchini Kenya na natazamia kujivunia kipindi kizuri nikiwa kocha wa kikosi hiki,” akasema Oliveira akiwa mwingi wa shukrani kwa usimamizi wa Gor Mahia kumwajiri.

“Gor Mahia wamejishindia takriban kila taji katika soka ya Kenya. Nahisi kwamba huu ndio wakati wanapostahili kudhihirisha ukubwa wa uwezo wao katika jukwaa la kimataifa kwenye mapambano ya CAF Champions League na CAF Confederations Cup.”

“Ili kufaulu katika hili, ni lazima kuwepo kwa ushirikiano mkubwa kati ya wachezaji, maafisa wa benchi ya kiufundi, mashabiki na usimamizi wa kikosi. Naamini hilo ni jambo linalowezekana,” akasema Oliveira.

You can share this post!

Wakulima wa majanichai Gatundu Kaskazini washabikia...

Ruiru, mtaa unaokua kwa kasi kufuatia kujengwa kwa Thika...