• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Gor Mahia yasema kuondoka kwa unyasi mmoja Odhiambo hakutavujisha nyumba yao

Gor Mahia yasema kuondoka kwa unyasi mmoja Odhiambo hakutavujisha nyumba yao

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Steven Polack wa Gor Mahia amesema kuondoka ka kipa chaguo la kwanza Peter Odhiambo hakutatikisa uthabiti wa kikosi chake.

Gor Mahia wamethibitisha kuagana rasmi na mlinda-lango huyo wa zamani wa Mathare United ambaye kwa sasa anahusishwa na uwezekano mkubwa wa kupata hifadhi mpya kambini mwa Wazito FC.

Wazito FC ya kocha Fred Ambani kwa sasa imesalia na kipa mmoja pekee – Bixente Otieno, baada ya kukatiza uhusiano na walinda-lango Steven Njung’e na Kevin Omondi.

“Odhiambo ameondoka Gor Mahia kwa maagano rasmi. Tunamshukuru kwa mchango wake ambao umetuwezesha kutamba katika soka ya humu nchini na majukwaa mengine ya kimataifa. Tunamtakia kila la heri katika maazimio yake ya baadaye,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Gor Mahia.

Mbali na Odhiambo, Gor Mahia wamethibitisha pia kuvunja ndoa na beki mzawa wa Tanzania, Dickson Ambundo aliyeingia katika sajili yao rasmi mwanzoni mwa msimu wa 2019-20 kwa mkopo kutoka kikosi cha Alliance FC, Tanzania.

Ambundo tayari amerejea kwao Tanzania anakohusishwa na uwezekano wa kutua Yanga SC ambao ni watani wa tangu jadi wa Simba SC katika Ligi Kuu ya Tanzania.

Hadi alipojiunga na Gor Mahia, Odhiambo alikuwa pia ameongoza kikosi cha 100o Street kutwaa ufalme wa kipute cha Koth Biro mnamo 2017.

Katika juhudi za kuziba pengo la Odhiambo, Gor Mahia tayari wamemsajili kipa Levis Opiyo kutoka Nairobi City Stars japo atalazimika kukabiliana vilivyo na ushindani mkali kutoka kwa kigogo Boniface Oluoch na David Mapigano ambaye ni mzawa wa Tanzania.

Polack amefichua pia mipango ya kujinasia huduma za wanasoka watatu zaidi wa haiba kubwa kadri anavyojiandaa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya na kutikisa miamba wa Afrika katika soka ya Klabu Bingwa Barani (CAF Champions League) msimu ujao.

“Itatulazimu kujisuka upya haraka iwezekanavyo baada ya kuweka wazi maazimio ya muhula ujao. Tayari tumetambua idara zinazohitaji kuimarishwa na tumetambua wanasoka walio na uwezo wa kutuzibia mapengo yaliyopo,” akasema kocha huyo mzawa wa Uingereza na raia wa Finland.

Ingawa Polack amesisitiza kwamba asingependa kabisa kupoteza mchezaji yeyote mwingine kambini mwake muhula huu, huenda ikawawia vigumu miamba hao kuwazuilia baadhi ya wanasoka wanaoelekezewa ofa nono kwingineko.

Mbali na nahodha Kenneth Muguna anayemezewa na miamba wa Tanzania, Simba SC, masogora wengine wanaotazamiwa kukatiza uhusiano wao na Gor Mahia ni naibu nahodha Joash Onyango, beki Charles Momanyi na mshambuliaji Nicholas Kipkurui.

Onyango aliyejiunga nao mnamo 2017 anahemewa sana na Simba SC ambao pia waliwahi kunyakua mvamizi Meddie Kagere na kiungo Francis Kahata kutoka Gor Mahia.

You can share this post!

Kizaazaa Nairobi spika Beatrice Elachi akijifungia ofisini

Nzoia Sugar sasa kupokea fedha za udhamini baada ya...

adminleo