• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:55 PM
Gor Mahia yateua kocha Sammy ‘Pamzo’ Omollo wa Posta Rangers kusimamia mechi zao za CAF Champions League

Gor Mahia yateua kocha Sammy ‘Pamzo’ Omollo wa Posta Rangers kusimamia mechi zao za CAF Champions League

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA mara 19 wa Ligi Kuu ya Kenya sasa wamemteua kocha Sammy ‘Pamzo’ Omollo wa Posta Rangers kushikilia mikoba yao kwenye kampeni za Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) msimu huu.

Gor Mahia wamepangiwa kuondoka humu nchini Jumatano kuelekea Kigali, Rwanda kwa gozi la mkondo wa kwanza wa mchujo wa CAF Champions League dhidi ya APR uwanjani Amahoro mnamo Novemba 28, 2020.

Kuteuliwa kwa Pamzo kunachochewa na tukio lililomshuhudia kocha mpya wa Gor Mahia, Roberto Oliveira akipigwa marufuku ya kusimamia mechi za CAF Champions League katika msimu wa 2020-21 kwa sababu ya kukosa cheti cha leseni ya kiwango cha Caf A au Cheti cha Uefa Pro ambacho ni cha kiwango sawa na cha Caf A.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), hayo ndiyo mahitaji ya msingi kwa mkufunzi wa kikosi chochote cha CAF Champions League kuwa nayo.

Uteuzi wa Pamzo ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Tusker FC, umethibitishwa na mwenyekiti wa Gor Mahia, Ambrose Rachier kwenye mtandao wa miamba hao wa soka ya humu nchini. Pamzo aliwahi kuwa mchezaji wa Gor Mahia katika kipindi chake cha usogora.

“Tutamtegemea Pamzo kushikilia mikoba ya Gor Mahia nchini Rwanda wakati ambapo tunajaribu kutafutia suluhu suitafahamu iliyoko kati ya Oliveira na CAF. Ina maana kwamba Pamzo atakuwa kinara wa benchi ya kiufundi dhidi ya APR nchini Rwanda kwa kuwa Oliveira haruhusiwi kusimamia mchuano wowote wa CAF Champions League kwa sasa,” akasema Rachier.

Maandalizi ya Gor Mahia ambao wanahitaji zaidi ya Sh4 milioni ili kufanikisha mchuano wao dhidi ya APR yametatizwa na mgomo baridi wa wachezaji ambao wamekuwa wakidai kulipwa malimbikizi ya mishahara.

Gor Mahia watakuwa wenyeji wa gozi la marudiano dhidi ya APR mnamo Disemba 5, 2020, jijini Nairobi. Mshindi wa michuano ya mikondo miwili kati ya Gor Mahia na miamba hao wa Rwanda atakutana ama na El Nasr ya Libya au mabingwa wa Algeria, CR Belouizdad.

Gor Mahia walichuana na APR kwa mara ya mwisho mnamo 2014 kwenye hatua ya makundi ya kipute cha Cecafa Kagame Cup na kuambulia sare ya 2-2 nchini Rwanda.

You can share this post!

Kosgei atiwa kwenye orodha ya wanariadha watakaonogesha...

Mfanyakazi wa zamani wa shirika lisilo la kiserikali aeleza...