• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 4:33 PM
Gor Mahia Youth, CMS Allstars, Butterfly na Tandaza wamenyania ubingwa

Gor Mahia Youth, CMS Allstars, Butterfly na Tandaza wamenyania ubingwa

 

Na JOHN KIMWERE

KIDUMWEDUMBE cha Ligi ya Taifa Daraja la Pili msimu huu kinaendelea kuwasha moto kwenye mechi za makundi yote tatu A, B na C. Michuano hiyo ya kutafuta tikiti ya kufuzu kupandishwa ngazi kushiriki Daraja la Kwanza msimu mpya imeibua ushindani mkali muhula huu.

Mfano kwenye mechi za Kundi C, farasi wanne ambao ni Gor Mahia Youth, CMS Allstars, Butterfly FC na Tandaza FC wanaendelea kutesa kubaini gani itabeba ubingwa huo.

Gor Mahia Youth ambayo hunolewa na kocha, Tom Ogweno inapiga mziki wa aina yake baada ya kukamata usukani wa kipute hicho kwa muda sasa, ambapo imefikisha pointi 45.

Nazo Butterfly FC, Tandaza FC na CMS Allstars zinakuja kwa kasi huku kila moja ikilenga kuibuka kidedea ili kusonga mbele.

Kwenye jedwali ya kipute hicho, baada ya CMS Allstars kuchoma MKU Thika mabao 2-1 wiki iliyopita inafunga mbili bora kwa alama 39, moja mbele ya Butterfly FC.

‘Kampeni za muhula huu kamwe siyo mteremko timu zote zimeonyesha zinajituma mithili ya mchwa kwenye jitihada za kusaka taji hilo,” meneja wa Butterfly, Fredrick Ndinya alisema na kuongeza kuwa siyo rahisi kubashiri timu itakayobeba ubingwa huo.

Ofisa huyo anasema jinsi hali ilivyo hakuna timu inayotarajia kupoteza mechi yoyote kati ya zilizosalia. Timu zote nne kila moja inapiga hesabu ndefu hasa kushinda mechi zote sijazo kujiongezea tumaini la kuibuka kileleni.

Timu zitakaomaliza nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Kundi A, B na C zitajiweka pazuri kujikatia tiketi ya kusonga mbele.

Baada ya kuibuka nafasi ya kwanza timu zote tatu zitacheza ‘Playoffs’ ambapo kila moja itapiga mechi mbili kupata nafasi ya kwanza hadi tatu na kusubiri FKF kutoa idadi itakayoafikiwa kusonga mbele.

‘Siwezi kubashiri hatima ya timu yangu maana tuna shughuli zito kwenye mechi sijazo,” alisema na kudai kuwa licha ya kukosa washambuliaji wazuri kikosi chake kimekaa vizuri kutifua vumbi kali.

Timu hiyo ina mechi nne ngumu inazolenga kushinda ili kuanza kutafakari inapoelekea. Butterfly FC ina vita dhidi ya Gogo Boys mchezo uliovurugwa na mvua wiki iliyopita. Baadaye Butterfly ya kocha, Bernard Shikuri imepangiwa kucheza na Tandaza FC kabla ya kutifuana na Spitfire FC.

Naye ofisa wa Gor Mahia Youth, George Onyango anasema wachana nyavu wao hawana la ziada mbali wameapa kuendelea kushusha soka la kufa mtu maana wanataka tiketi ya kusonga mbele msimu mpya.

”Jamani hatutaki kuishi kushiriki Daraja ya pili tumecheza kipute hicho kwa muda mrefu hata mavazi hubadilishwa tunataka kupandishwa ngazi msimu ujao,” ofisa huyo alisema na kuongeza kuwa wamepania kuendeleza mtindo wao kutembeza vipigo dhidi ya wapinzani wao.

Gor Mahia Youth imepoteza mchezo mmoja pekee ndani ya mechi 18 ilizoshiriki. Wanasoka wa kikosi hicho wameshinda mechi 14 kisha kutoka nguvu sawa mara tatu.

Gor Mahia Youth imepangwa kumenyana na Wajiji FC, Karatina Homeboys, Mathaithi FC kisha kuonana macho kwa uso na CMS Allstars mchezo unaopigiwa chapuo kuwa mgumu.

You can share this post!

Berlin FC macho kwa taji la Chapa Dimba

QUEEN NKIROTE: Sanaa iendelee kuvumishwa shuleni

adminleo