• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:50 AM
Gor Mahia Youth walambishwa sakafu, Butterfly waangusha Mathaithi

Gor Mahia Youth walambishwa sakafu, Butterfly waangusha Mathaithi

Na JOHN KIMWERE

WANASOKA wa Butterfly FC walipiga hatua walipofanikiwa kuangusha Mathaithi FC kwa mabao 2-1 kwenye mechi ya Kundi C Ligi ya Taifa Daraja ya Pili iliyochezewa katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Githunguri.

Nao limbukeni wa Gor Mahia Youth waliona giza walipokubali kuzimwa kwa mabao 2-0 na Maafande wa Spitfire kwenye patashika iliyopigiwa uwanja wa Moi Base, Nairobi.

Vijana wa Butterfly ya kocha, Bernard Shikuri walishuka dimbani tayari kuonyesha soka safi na kulipiza kisasi baada ya kulimwa kwa mabao 2-1 na Karatina Homeboys kwenye patashika iliyochezwa katikati mwa wiki.

Nahodha Evans Nakitare aliongoza wenzake kuingia mzigoni kufunza wapinzani wao soka na kufaulu kuhimili makali yao. Mpigagozi mwepesi Ibrahim Chimwani na Evans Nakitare kila mmoja alitikisa nyavu mara moja na kubeba Butterfly kuzoa alama tatu muhimu.

”Licha ya upinzani mkali tulifanikiwa kupiga gozi sawasawa na kuzoa alama zote na kujiongezea tumaini la kusonga mbele,” meneja wa Butterfly, Fredrick Ndinya alisema.

Nao mahasimu wao Tandaza FC ilijikuta njia panda ilipogaragazwa kwa bao 1-0 na Gogo Boys lililofumwa kimiani na Clinton Obasanjo. Kwenye mchezo mwingine, David Aura na Delyne Mayungu kila mmoja alipiga moja safi na kusaidia Bomas of Kenya kunasa ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Kibera United.

Kwenye mfululizo wa matokeo ya michuano hiyo, MKU Thika ilipigwa mabao 2-1 na Gathanga FC huku CMS Allstars ikiandikisha ushindi wa mabao idadi kama hiyo dhidi ya Karatina Homeboys.

  • Tags

You can share this post!

Ushuru FC wazimwa na Talanta

MTG waridhika na pointi nne baada ya mechi mbili

adminleo