Gor yacharaza Homeboyz na kuimarika ligini
Na JOHN ASHIHUNDU
BAADA ya kuibwaga Homeboyz 2-1 mnamo Alhamisi katika mechi ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) iliyochezewa Kenyatta Stadium mjini Machakos, Gor Mahia wamepanda kutoka nafasi ya nne hadi nambari mbili jedwalini.
Mabingwa hao watetezi walidhihirisha uwezo wao baada ya kucheza mechi hiyo bila nyota wao kadhaa waliogoma kutokana na kucheleweshwa kulipwa kwa marupurupu na mshahara wao wa mwezi Februari.
Kutokana na mgomo huo, Gor Mahia waliweza tu kwenda Machakos na wachezaji 15, ambapo 11 walianza kikosini huku wanne wakibakia kwenye benchi. Kinda Eric Ombija ni miongoni mwa waliopata nafasi kuanza kwa mara ya kwanza.
Nyota pekee walioanza kikosini jana ni nahodha Harun Shakava, Nicholas Kipkurui, Ernest Wendo, George Odhiambo na Lawrence Juma.
Mastaa ambao hawakuwa kikosini ni Francis Kahata, Jacques Tuyisenge, Samuel Onyango na Dennis Oliech.
Hata hivyo, huenda wakaanzishwa Jumapili katika mechi ya kimataifa dhidi ya Petro Atletico ya Angola katika mechi ya marudiano ya michuano ya Confederations Cup.
Ushindi
Baada ya Atletico kuibuka na ushindi wa 2-1 katika mkondo wa kwanza, lazima Gor Mahia washinde Jumapili ili wafuzu kwa robo-fainali ya michuano hiyo ya bara.
Gor Mahia walicheza mechi ya jana bila kufanya mazoezi tangu wakabiliane na Zamalek ya Misri katika mechi ya Kundi D mwishoni mwa wiki na kulimwa 4-0.
Katika mechi ya Alhamisi, Homeboyz walitangulia kupata bao kupitia kwa Luke Namanda dakika ya 50 kabla ya Francis Mustafa na Boniface Omondi kufungia KāOgalo ambao wamecheza mechi chache.
Licha ya kuingia uwanjani bila mazoezi, Gor Mahia walionyesha kiwango cha juu, ingawa wapinzani wao walipewa asilimia 53 ya umiliki wa boli dhidi ya 47 kwa Gor Mahia.
Baada ya kujibwaga uwanjani mara 18, Sofapaka wanaongoza msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 33 huku wakifuatiwa na Gor Mahia, na Bandari ambazo zote zimefikisha pointi 32.
Jumapili, Gor Mahia watakuwa bila winga matata Samuel Onyango kutokana na adhabu ya CAF.
Kadhalika, huenda kocha Hassan Oktay akamkosa kiungo mahiri, Kenneth Muguna kwenye mechi hiyo kutokana na jeraha linalomuandama.