• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
Gor yajawa na baridi Tusker, Bandari zikija kwa fujo KPL

Gor yajawa na baridi Tusker, Bandari zikija kwa fujo KPL

NA CECIL ODONGO

NI dhahiri kuwa mbio za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu (KPL) sasa utakuwa wenye ushindani baada ya viongozi Gor Mahia kupoteza wikendi, huku Tusker na Bandari zikizishinda mechi zao.

Mechi za KPL zimechukua mapumziko ya wiki mbili kupisha wiki za mechi za kimataifa kulingana na kalenda ya Fifa.

Baada ya kipindi hicho, raundi ya 16 ya MozzartBet Cup itasakatwa kabla ya mechi za KPL kurejelewa Aprili 6, 2024.

K’Ogalo walilambishwa kichapo cha 1-0 na Bandari huku Tusker ikimaliza rekodi ya AFC Leopards ya kutoshindwa katika mechi tisa.

K’Ogalo ina alama 50 huku Tusker na Bandari zikifuata kwa alama 43 japo Wanamvinyo hao wana ubora wa mabao.

Kichapo mikononi mwa Bandari kilikuwa cha pili kwa Gor msimu huu baada ya timu hiyo kupigwa 3-1 na Kenya Police mnamo Februari 3 msimu huu.

Kilijiri wiki mbili tu baada ya Gor kulazwa na Denmark FC 5-4 kupitia mikwaju ya penalti na kubanduliwa katika Kombe la MozzartBet.

Kusuasua kwa K’Ogalo kunaonyesha kuwa bado mbio za kuwania ubingwa wa KPL ziko wazi.

Hii ni kwa sababu wapinzani wameanza kuamini K’Ogalo si timu ngumu na inaweza kufungwa hata na timu zinazoshiriki ligi za chini kama Denmark.

Aidha, fomu ya Tusker inafaa kumtia Kocha Johnathan McKinistry wasiwasi kwa sababu Wanamvinyo hao huwa na mazoea ya kusajili matokeo mazuri KPL ikielekea ukingoni.

Tusker haijapoteza katika mechi nne zilizopita na mara ya mwisho ikipigwa KPL ni mnamo Februari 3 ilipolemewa 2-1 na Bidco United.

Gor ina mlima wa kukwea kwa kuwa itachuana na Kakamega Homeboyz nyumbani katika mechi yao ijayo mnamo Aprili 6 huku Tusker ikivaana na Kariobangi Sharks.

Iwapo Tusker itashinda nayo Gor idondoshe alama huenda ushindani ukaongezeka zaidi huku zikiwa zimesalia mechi 10 msimu utamatike.

Ubingwa ukizidi kuwa ngumu ndivyo navyo timu zinapambana kujinasua zisiteremshwe ngazi.

Itabidi wavuta mkia Nzoia Sugar na Shabana zijizatiti ili zisishushwe ngazi baada ya kujizolea alama 17 na 18 mtawalia.

Shabana imeshinda mechi moja tu tangu Kocha Sammy ‘Pamzo’ Omollo achukue usukani mnamo Januari 10 huku Nzoia ikilazimika kusaka huduma za kocha wa zamani Mike Muiruri kuokoa jahazi isizame mwishoni mwa msimu.

 

  • Tags

You can share this post!

Utata wa soko la Kombani wachacha

Kalonzo: Nilishinikiza Kibaki kumteua Kenyatta kama Naibu...

T L