Michezo

Green Commandos iko makini kunoa wachezaji wake vilivyo

March 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

KLABU ya soka ya Green Commandos ya Shule ya Upili ya Wavulana ya Kakamega imefanyia mabadiliko makubwa mazoezi yake ili kutoa mafunzo ya hali ya juu kwa wachezaji wake.

Commandos, ambao wamekuwa wakichangia pakubwa katika ukuzaji wa talanta katika soka ya Kenya tangu mwaka 1979, sasa wanatafuta makocha wazoefu kutoka mataifa mengine ili kukuza machipukizi katika shule hiyo.

Mwezi Desemba 2019, Commandos ilizuru Nairobi kwa mafunzo ya wiki mbili yaliyofanyika katika klabu ya Public Service mtaani Upper Hill.

Mwenyekiti wa Green Commandos, Issac Kwoba, ameahidi kuwa mafunzo zaidi yamo mbioni wakati wa likizo.

“Tutakuwa na mafunzo ya majuma mawili wakati wa likizo ya Desemba katika klabu ya Public Service jijini Nairobi na pia mjini Kakamega. Tunaamini kwa kufanya hivyo, tutaweza kutambua vipaji zaidi kabla ya kuanza kuvikuza,” afisa huyo alisema katika mahojiano ya kipekee.

Katika kambi ya mafunzo iliyopita, wanafunzi 65 walifika Public Service na kupata mafunzo kutoka kwa kocha wa timu ya taifa ya Poland ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 23, Marek Dragosz.

Green Commandos, ambayo ndio timu ya kwanza kutoka shule kushiriki Ligi ya Supa, pia inatumia wachezaji wa zamani wa timu za taifa na makocha watajika.

Ilianzishwa miaka ya 1970 kama kituo cha kukuza talanta chini ya kocha wa zamani wa Harambee Stars Bernard Zgoll kutoka Ujerumani na Mkenya Jonathan Niva. Ilipata kuimarishwa zaidi chini ya kocha Christopher Makokha.

Baadhi ya majina makubwa yaliyopitia Green Commandos ni Dan Musuku, Peter Lichungu, Reginald Asibwa, Antony Fwaya, Edward Seda, John Okello Zangi, Joash Okongo, Mike Otieno, Ronald Wathiera na Isaac Kwoba.

“Hakuna timu nchini Kenya ambayo haina wachezaji waliopitia Green Commandos. Tulikuwa na wachezaji 11 katika timu ya taifa ya Under-20. Klabu ya Kariobangi Sharks ina wachezaji sita kutoka hapa, Ulinzi Stars wanne na AFC Leopards sita,” alisema Kwoba.

“Bado tunaendelea kukuza talanta inayoaminika jinsi mlivyoshuhudia timu ya Kariobangi Sharks ikibwaga Everton kutoka nchini Uingereza mwaka 2019 ikiwa na wachezaji tisa waliopitia katika mikono yetu akiwemo kocha Edward Seda,” aliongeza.

Wanasoka waliopitia Kakamega High wamekuwa mfano bora kiasi cha kuwapa machipukizi wengi motisha ya kufuata nyayo zao.

“Nataka kusakata soka yangu barani Ulaya. Nataka kung’ara kama wachezaji waliopitia hapa,” alisema mwanafunzi wa kidato cha tatu Maxwell Odada katika mahojiano.

Odada alipuuzilia mbali dhana kuwa wanafunzi wanaozamia michezo hawawezi kufanya vyema katika masomo yao.

“Wengi wamesoma hapa na kupata alama ya juu (A) pamoja na kujitokeza kuwa wachezaji wazuri sana. Hapa tunafuata ratiba ya shule kama tu wengine. Hata hivyo, nidhamu ni kitu cha maana.”