• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 5:01 PM
Griezmann kuwa nguzo na tegemeo la Barcelona chini ya kocha Koeman

Griezmann kuwa nguzo na tegemeo la Barcelona chini ya kocha Koeman

Na MASHIRIKA

KOCHA Ronald Koeman amesema fowadi Antoine Griezmann ndiye atasalia mwanasoka nguzo atakayetegemewa na Barcelona kadri kikosi hicho kitakavyopania kujisuka upya kwa minajili ya kampeni zijazo.

Barcelona tayari wamefichua azma ya kuagana rasmi na mshambuliaji Luis Suarez huku wakitazamiwa pia kukatiza uhusiano na nahodha Lionel Messi anayehusishwa pakubwa na Manchester City, PSG na Inter Milan.

Suarez kwa upande wake anawaniwa pakubwa na Juventus na Atletico Madrid.

Kwa mujibu wa wakala Eric Olhats, Griezmann alikuwa tayari kuondoka ugani Camp Nou mwishoni mwa msimu huu baada ya kulazimika kucheza katika nafasi ambayo hajaizoea kila mara alipowajibishwa kwa pamoja na Messi na Suarez kambini mwa Barcelona.

“Alishiriki kikao na Koeman ambaye kwa sasa amemhakikishia kwamba atamchezesha katika nafasi inayomfaa zaidi ugani,” akasema Olhats.

Griezmann ambaye ni mzawa wa Ufaransa, alisajiliwa na Barcelona kutoka Atletico kwa kima cha Sh14 bilioni mwanzoni mwa msimu huu wa 2019-20.

Hata hivyo, hakuridhisha jinsi ilivyotarajiwa huku akichezeshwa kwa dakika zote 90 za mechi moja mara 19 pekee.

Chini ya wakufunzi Ernesto Valverde na Quique Setien waliopigwa kalamu na Barcelona msimu huu, Griezmann alifunga mabao 15 pekee kutokana na mechi 48.

“Alikuwa amefikia maamuzi ya kuagana na Barcelona hata kabla ya mechi ya robo-fainali ya UEFA iliyowashuhudia wakipigwa 8-2 na Bayern Munich. Dalili zote ziliashiria kwamba hakuwa sehemu ya mipango ya klabu na hakuwa katika mawazo ya kocha. Hata hivyo, kwa sasa yuko radhi kusalia Camp Nou na Koeman atamuunga mkono kwa mengi,” akaongeza Olhats.

Kwa mujibu wa gazeti la L’Equipe, Griezmann kwa sasa watavalia jezi nambari saba mgongoni badala ya 17 msimu ujao, ishara kwamba huenda kiungo Philippe Coutinho ambaye amekuwa kambini mwa Bayern Munich kwa mkopo kutoka Barcelona, hana mipango ya kurejea ugani Camp Nou.

“Kwa heshima zote, Griezmann lazima arejee kucheza katika nafasi aliyozoea kambini mwa waajiri wake wa zamani na timu ya taifa. Hapa ndipo msaada na ushauri wa kocha unahitaji zaidi,” akasema Koeman.

You can share this post!

Olunga, Johanna na Wanyama wafurahisha waajiri wao katika...

Leeds United wavunja benki na kumng’oa Rodrigo Moreno...