Michezo

GSU yakosa makali ya kuingia robo-fainali voliboli ya Afrika

April 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa voliboli ya wanaume nchini Kenya, General Service Unit (GSU) wamekataa tamaa ya kufika robo-fainali ya mashindano ya Klabu Bingwa Afrika yanayoendelea jijini Cairo nchini Misri baada ya kuandikisha ushindi mmoja na kupokezwa vichapo viwili kwenye Kundi D.

Maafisa hawa wa polisi, ambao walinyakua medali ya shaba mwaka 2005 nchini Benin, watakutana na University of Zimbabwe mnamo Aprili 5 na kumaliza mechi za makundi dhidi ya Mwangaza kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mnamo Aprili 6.

Katika mahojiano na Taifa Leo Dijitali mnamo Alhamisi, kocha Gideon Tarus amesema, “Tulianza mashindano vibaya kwa kupoteza mechi mbili (dhidi ya Assaria kutoka Libya na Nemo Stars ya Uganda).

Tulipata ushindi katika mechi ya tatu (dhidi ya AS Fag kutoka Guinea), lakini tuko tayari kukabiliana na Univeristy of Zimbabwe. Timu ya Zimbabwe ni timu nzuri.

Tutajitahidi kucheza vyema. Kuhusu uwezo wetu wa kufika robo-fainali ni kwamba hatutaweza kufika awamu hiyo. Tumecheza vibaya sana mashindano haya na tutang’ang’ana kumaliza nafasi ya tisa and hatuna budi kukubali hilo.”

Wawakilishi wengine kutoka Kenya katika mashindano haya yaliyovutia timu 22 ni Prisons. Vijana wa kocha David Lung’aho walifufua matumaini ya kuingia robo-fainali baada ya kutoka chini seti moja na kucharaza FAP kutoka Cameroon 3-2 (15-25, 25-15, 15-25, 25-17, 15- 8) katika Kundi C.

Prisons ilianza kampeni kwa kulima Wolaita kutoka Ethiopia 3-0 kabla ya kupigwa breki na Al Swehly kutoka Libya kwa seti 3-1.

Timu mbili za kwanza kutoka makundi A, B, C na D zitaingia robo-fainali. Prisons inashikilia nafasi ya pili katika kundi C nayo GSU ni nambari tatu katika kundi D. Mabingwa watetezi ni wenyeji Al Ahly ambao wanafukuzia taji lao la 14. Leo Alhamisi imekuwa siku ya mapumziko.