• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 9:50 AM
GUU 16-BORA: Nigeria, Misri guu ndani ya 16-bora wakishinda

GUU 16-BORA: Nigeria, Misri guu ndani ya 16-bora wakishinda

CAIRO, MISRI

NIGERIA, Misri na Uganda watakuwa wa kwanza kufuzu kwa hatua ya mwondoano katika fainali za Kombe la Mataifa Bingwa barani Afrika (AFCON) mwaka 2019 iwapo watawazamisha Benin, DR Congo na Zimbabwe mtawalia katika mechi za Juni 26, 2019.

Timu mbili za kwanza zitakazotawala vilele vya makundi yote sita zitatinga raundi ya 16-bora moja kwa moja, huku vikosi vinne vingine vitakavyokamilisha mechi za makundi katika nafasi za tatu kwa kujizolea alama nyingi zaidi pia vikijikatia tiketi.

Wenyeji Misri watashuka katika uwanja wa Kimataifa wa Cairo kuchuana na DR Congo wakijivunia hamasa tele baada ya kuanza vyema kampeni zao za Kundi A kwa ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Zimbabwe mnamo Ijumaa iliyopita.

Mchuano huo utasakatwa saa tano usiku baada ya Uganda kupimana ubabe na Zimbabwe katika kivumbi hiki cha Kundi A mwendo wa saa mbili usiku.

Mbali na kuchuma nafuu ya wingi wa mashabiki wao wa nyumbani, Misri ambao wanasaka taji lao la nane la AFCON na la kwanza tangu mwaka wa 2010, wanatazamiwa pia kutambishwa zaidi na mvamizi matata wa Liverpool, Mohamed Salah.

Salah ambaye alitawazwa Mwanasoka Bora wa Afrika mnamo 2017 na 2018, alikuwa sehemu muhimu katika kikosi cha Misri dhidi ya Zimbabwe wiki jana, huku kasi yake ikiwa kiini cha kuhisika zaidi kwa ushawishi wake uwanjani.

Zaidi ya kumtatiza kipa Edmore Sibanda na mwenzake Elvis Chipezeze aliyewajibishwa katika dakika ya 13 baada ya Sibanda kujeruhiwa, Salah alichangia krosi iliyokamilishwa kwa ustadi na fowadi Mahmoud ‘Trezeguet’ Hassan kunako dakika ya 41.

Ushindi mara saba wa taji la AFCON ni rekodi inayofanya Misri kuwa kikosi kinachojivunia ufanisi mkubwa zaidi katika historia ya kipute hicho.

Kwa upande wao, Uganda ndio kwa sasa wanaobeba tumaini kubwa la vikosi vya Afrika Mashariki baada ya Kenya, Tanzania na Burundi kupoteza mechi zao za ufunguzi wa makundi.

Chombo cha Kenya kiliyumbishwa na Algeria kwa mabao 2-0 mnamo Jumapili, saa chache baada ya Senegal pia kuwazamisha Tanzania kwa kichapo sawa na hicho.

Burundi waliowadhibiti Nigeria hadi dakika za mwisho, walizidiwa maarifa na mchezaji Odion Ighalo aliyetokea benchi katika dakika za lala-salama na kuwafungia Super Eagles bao la ushindi katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi B mnamo Jumamosi.

Chini ya mkufunzi Sebastien Desabre, Uganda waliwapepeta DR Congo 2-0 katika mchuano wao wa kwanza wa Kundi A.

Mabao ya Uganda yalifumwa wavuni kupitia kwa wachezaji Patrick Kaddu na Emmanuel Okwi ambao kwa mara nyingine, wanatazamiwa kuwa tegemeo kubwa la Desabre ambaye ni mzaliwa wa Ufaransa.

Ushindi wa Uganda dhidi ya DR Congo waliotawazwa mabingwa mnamo 1968 na 1974, ulikuwa wa kwanza kwa kikosi hicho cha Afrika Mashariki kuwahi kusajili katika fainali za AFCON tangu 1978 walipoambulia nafasi ya pili.

Uganda na Misri kwa sasa wanaselelea kileleni mwa Kundi A kwa alama tatu kila mmoja, huku Zimbabwe na DR Congo wakisalia bila alama yoyote.

Katika Kundi B, Nigeria wanadhibiti usukani kwa alama tatu, mbili zaidi kuliko Guinea na Madagascar waliotoshana nguvu baada ya kuambulia sare ya 2-2 mnamo Jumamosi.

Wakati uo huo, beki tegemeo wa Nigeria anayeuguza jeraha ni miongoni mwa wachezaji watatu wa Super Eagles waliokosa kufanya mazoezi jana kwa ajili ya pambano la kesho dhidi ya Guinea ya kocha Paul Put.

Shehu Abdullahi, Jamilu Collins na Samuel Kalu hawakuwa mazoezini jana wakati kikosi hicho cha kocha Gernot Rohr kilijiandalia katika uwanjani ambao mashabiki hawakuruhusiwa kuingia.

Ushindi dhidi ya Guinea utawahakikishia vijana hao wa nafasi katika hatua ya 16 Bora, baada ya ushindi mwingine wa awali wa 1-0 dhidi ya Burundi katika mechi ya ufunguzi.

Mshambuliaji Odion Ighalo anayepewa nafasi kubwa ya kufanya vyema na kuisaidia timu hiyo kusonga mbele alionekana kuwa katika hali njema zaidi mazoezini.

Lakini beki Abdullahi aliyeondolewa uwanjani baada ya kuumia wakicheza na Burundi, huenda akaikosa mechi ya leo dhidi ya Guinea ambayo ilifuzu kwa michuano hii bila kushindwa.

  • Tags

You can share this post!

Mali yaponda Mauritania, Angola wakiyumbisha dau la Tunisia

Matamshi ya Jaguar yakoroga mambo mataifa jirani

adminleo