Michezo

Haaland afungia Dortmund mabao manne huku chipukizi Muokoko akiweka rekodi Bundesliga

November 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

ERLING Braut Haaland, 20, alifunga mabao manne katika kipindi cha pili na kusaidia Borussia Dortmund kutoka nyuma kwa goli moja na kuponda Hertha Berlin 5-2 katika mechi ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) mnamo Novemba 21, 2020.

Ushindi huo wa Dortmund uliwasaidia kupunguza pengo la alama kati yao na viongozi Bayern Munich hadi pointi moja pekee baada ya mabingwa hao watetezi kulazimishiwa sare ya 1-1 na Werder Bremen ugani Allianz Arena.

Halaand ambaye ni raia wa Norway alifunga mabao matatu chini ya dakika 15 na kuweka hai matumaini ya Dortmund ya kuzima ukiritimba wa Biayern katika gozi la Bundesliga.

Raphael Guerreiro aliwafungia Dortmund goli la nne katika dakika ya 70 kabla ya Haaland kukamilisha karamu ya mabao kwa upande wa waajiri wake kunako dakika ya 79.

Hertha walifutiwa machozi na Matheus Cunha wa Brazil aliyecheka na nyavu za wageni wao katika dakika za 33 na 80. Mchuano huo ulimpa kocha Lucien Favre fursa ya kumwajibisha chipukizi Youssoufa Moukoko.

Siku moja baada ya kuadhimisha umri wa miaka 16, Muokoko aliweka historia ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kiunri kuwahi kuwajibishwa katika kampeni za Bundesliga.

Kinda huyo mzawa wa Cameroon na raia wa Ujerumani aliyeletwa ugani katika dakika tano za mwisho, anajivunia kufunga jumla ya mabao 141 kutokana na mechi 88 ambazo amechezea kikosi cha chipukizi wa Dortmund.

Haaland kwa sasa amepachika wavuni jumla ya mabao 10 kutokana na mechi sita zilizopita ambazo amechezea Dortmund katika mapambano yote na amefunga mabao 21 kutokana na michuano 17 ambayo amecheza katika ngazi ya klabu na timu ya taifa.

Nyota huyo alitawazwa Chipukizi Bora wa Mwaka wa 2020 baada ya kutwaa taji la Golden Boy miongoni mwa wanasoka wasiozidi umri wa miaka 21 kutoka Ligi Kuu za mataifa ya bara Ulaya mnamo Novemba 21, 2020. Alimpiku Ansu Fati wa Barcelona na timu ya taifa ya Uhispania pamoja na Alphonso Davies wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Canada walioambulia nafasi za pili na tatu mtawalia kwenye vita vya kuwania taji hilo.

Hata hivyo, mwishoni mwa mechi iliyowakutanisha na Hertha, Haaland alikuwa mwingi wa sifa kwa Muokoko akimtabiria mambo makuu katika ulingo wa soka.

“Ningependa zaidi kupata fursa nyingi za kucheza pamoja naye. Ni miongoni mwa chipukizi wanaojivunia utajiri mkubwa wa vipaji katika soka. Katika umri wa miaka 16 pekee, amedhihirisha ukubwa wa uwezo alio nao na angali na miaka mingi ya kutamba katika majukwaa ya kimataifa. Ni tija na fahari tele kwamba yeye ni sehemu ya kikosi cha sasa cha Dortmund,” akasema Haaland.

Hadi kivumbi cha Bundesliga kilipopisha mechi za kimataifa wiki iliyopita, Dortmund walikuwa wamepigwa 3-2 kwenye soka ya Bundesliga. Japo walijibwaga ugani wakitawaliwa na kiu ya kujinyanyua dhidi ya Hertha, walijipata nyuma kwa bao moja mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya Cunha kuwaweka waajiri wake uongozini katika dakika ya 33.

Hata hivyo, Haaland alisawazisha mambo dakika mbili pekee mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya kukamilisha kwa ustadi krosi ya kiungo Emre Can. Alicheka na nyavu za wageni wao dakika mbili baadaye kabla ya kufunga mawili mengine baada ya kushirikiana vilivyo na Jude Bellingham pamoja na Guerreiro.

Cunha alifungia Hertha bao la pili kupitia penalti ya dakika ya 79 na kufanya mambo kuwa 4-2 sekunde chache kabla ya Dortmund kufunga la tano. Ni matarajio ya Tuchel kwamba ushindi mnono uliosajiliwa na Dortmund dhidi ya Hertha sasa utawatabisha ipasavyo dhidi ya Club Bruges ya Ubelgiji katika mechi ya Klabu Bingwa Ulaya itakayowakutanisha mnamo Novemba 24, 2020 ugani Signal Iduna Park, Ujerumani.