Michezo

HAMNA SWALI! Liverpool watesi wakuu mkondo wa kwanza ukiisha

December 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL, UINGEREZA

KLABU ya Liverpool kwa sasa imeshinda mechi kumi na nane na kutoka sare katika mechi moja kati ya mechi 19 za mkumbo wa kwanza kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza msimu huu, kando na kutwaa Kombe la Dunia na kutazwa mabingwa wa Uefa Super Cup.

“Muhula wa 2019 ulikuwa mzuri lakini sio muhimu maana huwa tunahesabu misimu wala sio miaka lakini msimu wa 2019/2020 haujaisha,” asema kocha Jurgen Klopp.

“Ndio tumekamilisha mkondo wa kwanza huku zikisalia mechi 19 ambapo michezo 18 kati yazo huenda tukaandikisha matokeo ya usiku huu. Nani anajali kuhusu pointi mwezi Desemba? Tayari, tushatengeneza kanuni tunazopania kutumia kutoka sasa na kusonga mbele, ni hayo tu.”

Wachezaji wa Wolves hawakuwa na furaha hata kabla ya hitilafu za mtambo wa VAR. Sherehe za Krismasi zilimaanisha walitua katika uwanja wa Anfied takribani saa 45 tu baada ya kufuma Manchester City mabao 3-2. Katika mchezo huo walighadhabishwa na matukio mawili yaliyowapata katika kipindi cha kwanza.

Van Dijk alifuma pasi ndefu iliyotulizwa na Lallana kwa bega, kabla ya kuanguka na Mane akaipiga wavuni.

Awali refarii alikataa bao akisema Lallana alinawa lakini teknolojia ya VAR ikasema ni bao.

Hata hivyo, Wolves haikufurahishwa na hatua ya Virgil Van Dijk alivyodaiwa alikuwa amegeuza mtanange huo kuwa wa handiboli ilhali haikugunduliwa wakati alitenda kosa hilo.

Hayo yalitokea katika kipindi cha kwanza huku Pedro Neto akiona bao lake likifutiliwa mbali. Naye Jonny alikisiwa alikuwa ameotea akiwa hatua chache tu kufunga bao lingine katika kampeni za kinyang’anyiro cha msimu huu.

Kwingineko, Manchester City walifanikiwa kulipiza kisasi baada ya kulimwa na Wolves ilipofunika Sheffied United mabao 2-0 yaliyopatikana kupitia Sergio Aguero na Kevin de Bruyne. Mkufunzi wa Manchester City, Pep Guardiola alikuwa amelalamika kuhusu mpangilio wa pambano hali iliyochangia kung’oa nanga kabla ya saa 48 na kulazimisha kushirikisha kikosi kilichocheza mchezo uliopigwa Ijumaa ilipozabwa mabao 3-2 ugani Molineux. City ilionekana kuanza vizuri kipindi cha kwanza huku Blades akisakata gozi la kuvutia na kutengeneza nafasi nzuri za kufunga kabla bao lililofumwa na Lys Mousset kukataliwa baada ya mtambo wa VAR kuonyesha alikuwa ameotea.

Wachezaji walionyesha mchezo wa kujituma ambapo De Bruyne alishirikiana na Aguero na kufanikiwa kucheka na wavu dakika saba baada ya muda wa mapumziko. Kwa mara nyingine, De Bruyne alionyesha ukakamavu wake na kutumbia kambani bao lake dakika nane baadaye.

Matokeo hayo yalifanya kikosi cha Sheffield kukubali kichapo cha pili ugenini na kufanya City kuweka pengo la alama 14 baina yake na Liverpool ambayo hadi sasa ingali kidedea kwenye msimamo.