Harambee Starlets yaalika Zambia mechi ya kufuzu Olimpiki
Na CHRIS ADUNGO
MASHABIKI watakaofika uwanjani Kasarani kushabikia vipusa wa Harambee Starlets, katika mchuano wa kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki Tokyo, hawatatozwa kiingilio.
Starlets watamenyana na vipusa wenzao kutoka Zambia siku ya Ijumaa, katika juhudi za kujikatia tiketi ya kushiriki michezo hiyo ya Olimpiki itakayofanyika nchini Japan mwaka ujao.
Kwa mujibu wa vinara wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), kuondolewa kwa ada ya kiingilio ni uamuzi wa kimakusudi unaonuia kuvutia mashabiki wengi zaidi kutilia shime kikosi cha Starlets.
Mchuano huo utasimamiwa na refa Shamirah Nabaddah akisaidiwa na waamuzi wenzake wazawa wa Uganda – Jane Mutonyi, Nakitto Nkumbi na Florence Ayaro.
Aline Bitagoye kutoka Burundi na Agar Mezing wa Cameroon watakuwa makamishna wa pambano hilo. Starlets watajibwaga ugani siku tatu tu baada ya kupepetwa 3-1 na chipukizi wa Kenya wasiozidi umri wa miaka 15, katika mechi ya kirafiki iliyofanyika uwanjani Nyayo, Nairobi, mnamo Jumanne.
Hadi kufikia mwishoni mwa wiki jana, uchechefu wa fedha ulitishia kusambaratisha maandalizi ya Starlets baada ya FKF kuvunja kambi ya mazoezi ya vipusa hao, wanaonolewa na kocha David Ouma.
Ilimlazimu Waziri wa Michezo Amina Mohammed kuingilia kati huku FKF ikithibitisha kwamba, wote walioitwa kambini walikuwa wameripoti kufikia Jumatatu tayari kwa mazoezi ya kujifua.
Chini ya mkufunzi Ouma, Starlets wako pua na mdomo kuweka historia ya kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki kwa mara ya kwanza, iwapo watazamisha chombo cha Zambia baada ya michuano ya mikondo miwili.
Katika safari yao ya kufuzu hadi kufikia sasa, vipusa hao wa Kenya waliwabandua Ghana na Malawi. Ndio wanapigiwa upatu kuwakilisha bara Afrika nchini Japan mwaka 2020 baada ya miamba Afrika Kusini na Nigeria kudenguliwa.
Mchuano wa marudiano kati ya Kenya na Zambia utachezwa jijini Lusaka Jumatatu ijayo, Novemba 11.
Kikosi cha Harambee Starlets
Makipa: Annete Kundu (Eldoret Falcons), Judith Osimbo (Gaspo), Wilfrida Seda (Vihiga Queens), Monica Odato (Wadadia).
Mabeki: Vivian Nasaka (Vihiga Queens), Dorcas Shikobe (Oserian Ladies), Lydia Akoth (Thika Queens), Lucy Akoth (Mathare United), Ruth Ingosi (Eldoret Falcons), Wincate Kaari (Gaspo), Nelly Sawe (Thika Queens), Dorcas Shiveka (Eldoret Falcons), Sylvia Lumasia (Kibera Girls Soccer Academy).
Viungo: Jentrix Shikangwa (Wiyeta Girls), Cynthia Shilwatso (Vihiga Queens), Sheril Angachi (Gaspo), Corazone Aquino (Gaspo), Mwanalima Adam (Thika Queens), Elizabeth Wambui (Gaspo Women), Providence Kasiala (Wiyeta Girls). Washambuliaji: Topistar Situma (Vihiga Queens), Bertha Omita (Kisumu All Starlets), Mercy Airo (Kisumu All Starlets), Janet Bundi (Eldoret Falcons).