• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Harambee Starlets yatua Uturuki salama tayari kuvaana na Northern Ireland

Harambee Starlets yatua Uturuki salama tayari kuvaana na Northern Ireland

Na GEOFFREY ANENE

HARAMBEE Starlets ya Kenya itaanza kampeni yake kwenye makala ya tatu ya soka ya kimataifa ya Turkish Women’s Cup dhidi ya Northern Ireland B mnamo Machi 4, 2020.

Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), ambao wamefika salama salmini nchini humo Jumanne, kisha watapepetana na Chile (Machi 7) na kukamilisha mechi za Kundi B dhidi ya Uzbekistan mnamo Machi 10.

Droo ya mashindano haya ya mataifa manane ilifanywa mjini Alanya nchini Uturuki mnamo Februari 28.

Starlets ya kocha David Ouma ilitoka jijini Nairobi mapema Jumanne baada ya kuitikia mwaliko huo na kuwa mojawapo ya timu za kwanza kabisa kutoka Bara Afrika kushiriki mashindano hayo.

Black Queens ya Ghana, ambayo ni timu nyingine kutoka Afrika kualikwa kushiriki makala haya, pia iko katika kundi hilo. Dimba hili, ambalo pia hufahamika kama Alanya Gold City Cup, litang’oa nanga Machi 44 na kufikia kilele mnamo Machi 11. Kundi A linaleta pamoja Romania, Hungary, Venezuela na Hong Kong.

Katika viwango bora vya washiriki kwenye Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Chile inapatikana katika nafasi ya 36 duniani, Romania (43), Hungary (45), Northern Ireland (56), Venezuela (58), Ghana (60), Hong Kong (74) na Kenya (133).

Kenya inatumia mashindano hayo kujipiga msasa kabla ya kuanza kampeni yake ya kuingia Kombe la Afrika (AWCON) 2020. Itamenyana na Tanzania mwezi Aprili nyumbani na ugenini katika raundi ya kwanza.

Mshindi kati ya Kenya na Tanzania atakabiliana na mshindi wa mechi kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sao Tome & Principe katika raundi ya pili ambayo mshindi atajikatia tiketi ya kushiriki AWCON mnamo Novemba 23 hadi Desemba 20, 2020.

You can share this post!

Meno ya makinda wa Arsenal yapewa sifa

Kamworor kuongoza kikosi cha nusu marathon Poland

adminleo