Harambee Stars kupimana nguvu na Chipolopolo
Na CHRIS ADUNGO
KOCHA Francis Kimanzi anaamini kwamba kikosi chake cha Harambee Stars kitachuma nafuu kutokana na mchuano ujao wa kirafiki kabla ya mechi mbili za kufuzu kwa Kombe la Afrika (AFCON) 2021 iwapo serikali itatoa mapema utaratibu na mwongozo wa kurejelewa kwa michezo humu nchini.
Stars wamepangiwa kupimana nguvu na Zambia mwezi ujao kabla ya kushuka dimbani kuvaana na Comoros katika mechi za Kundi G za kufuzu kwa AFCON 2021 mnamo Novemba 9 nyumbani kisha Novemba 12 ugenini.
Kimanzi ameisihi serikali kupitia Wizara ya Michezo kulegeza baadhi ya kanuni na kuondoa marufuku yanayolenga kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 ili kuwapa Stars jukwaa mwafaka zaidi la kujiandaa kwa mapambano hayo yajayo.
Ingawa Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) alikuwa awali amedokeza kuhusu uwezekano wa Stars kupimana nguvu na Sudan mwanzoni mwa Oktoba kabla ya kupepetana na Comoros, imebainika kwamba Zambia ndio watakakwaruzana na Kenya kirafiki.
Mpango huo umefichuliwa na Shirikisho la Soka la Zambia (FAZ) ambalo kupitia mtandao wa Twitter, limethibitisha kwamba Stars ya Kenya na Bafana Bafana ya Afrika Kusini zitavaana na Chipolopolo ya Zambia katika mechi mbili za kupimana nguvu ugenini mwezi ujao.
“Tutacheza na Kenya jijini Nairobi kisha kusafiri Afrika Kusini kwa gozi la pili la kirafiki mwezi ujao,” ikasema sehemu ya taarifa hiyo ya FAZ.
Ni matumaini ya Kimanzi kwamba vijana wake, hasa wanaosakata soka ya humu nchini, watapata fursa ya kujiandaa mapema kabla ya kushiriki michuano hiyo mitatu katika kipindi cha miezi miwili ijayo.
Kocha huyo aliyewaongoza Mathare United kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) mnamo 2008, ameridhishwa mno na tukio la Stars kupanda kwa nafasi moja zaidi kutoka nambari 107 hadi 106 kwenye orodha ya viwango bora vya kimataifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) mnamo Septemba 17.
“Hizi ni habari za kutia moyo sana hasa ikizingatiwa kwamba hatujashiriki mchuano wowote kwa miezi kadhaa iliyopita. Sasa tuna changamoto kubwa ya kujitahidi hata zaidi kuimarika kwenye orodha hiyo,” akatanguliza.
“Tulifanya vyema kabla ya mkurupuko wa virusi vya corona. Janga hili limevuruga maandalizi yetu na itakuwa vyema iwapo serikali itatupa mwelekeo mapema ndipo FKF iitupe idhini ya kuwaita wanasoka kambini kwa minajili ya kampeni zilizopo mbele yetu,” akasema Kimanzi ambaye huenda akategemea sana masogora wanaopiga soka katika mataifa ya nje.
Hata hivyo, timu ya taifa ya wanawake almaarufu Harambee Starlets wameteremka kwa nafasi nne zaidi kutoka 133 hadi 137 kimataifa.
Stars kwa sasa inashikilia nafasi ya pili kwenye Kundi G la kufuzu kwa fainali za AFCON 2021. Stars wanajivunia alama mbili kutokana na sare za 1-1 dhidi ya Misri ugenini mnamo Novemba 14, 2019 na Togo nyumbani mnamo Novemba 19, 2019 katika mechi mbili za ufunguzi wa Kundi G.
Kwenye msimamo wa hivi karibuni wa FIFA, Ubelgiji wangali kileleni wakifuatwa na Ufaransa, Brazil na Uingereza. Senegal wanaongoza barani Afrika wakifuatwa na Tunisia, Nigeria na Algeria.