Harambee Stars roho mkononi droo ya Afcon ikitangazwa Cairo
Na GEOFFREY ANENE
DROO ya makala ya 32 ya Kombe la Afrika (AFCON) 2019 itafanyika mjini Giza nchini Misri Ijumaa saa tatu usiku saa za Kenya.
Harambee Stars, ambayo inashikilia nafasi ya 108 duniani, itafahamu wapinzani wake wa mechi za kundi kutoka chungu cha kwanza kinachojumuisha wenyeji Misri, ambao ni mabingwa mara sita, Cameroon (mabingwa watetezi), wanafainali wa mwaka 2002 Senegal, washindi wa mwaka 2004 Tunisia, Ghana na Ivory Coast ambao wanajivunia mataji mawili kila mmoja; chungu cha pili kinachoshirikisha Morocco, Nigeria, Algeria, Guinea, Mali na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na chungu cha tatu kinachojumuisha Uganda, Afrika Kusini, Guinea Bissau, Zimbabwe, Angola na Burundi.
Kenya iko katika chungu cha nne pamoja na Mauritania, Namibia, Benin, Madagascar na Tanzania. Haitarajiwi kukutana na wapinzani kutoka chungu cha nne katika mechi za makundi.
Mataifa haya 24 yatagawanywa katika makundi sita ya timu nne nne.
Misri pekee ndiyo inayofahamu kundi lake. Imetiwa katika Kundi A.
Cameroon, Ghana, Ivory Coast, Tunisia na Senegal pia zinatarajiwa kuongoza makundi yao droo itakapofanywa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).
Vyungu vinne vitakavyotumiwa katika droo viliundwa kutokana na ushiriki wa taifa katika AFCON mwaka 2013, 2015 na 2017, ushiriki wa taifa katika mechi za kufuzu kushiriki AFCON mwaka 2015, 2017 na 2019 na viwango vya soka vilivyotolewa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) majuzi.
Makala haya ya 32 yatafanywa kutoka Juni 21 hadi Julai 19.