• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 12:16 PM
Harambee Stars ya Kenya kucheza na Chipolopolo ya Zambia bila mashabiki ugani Nyayo

Harambee Stars ya Kenya kucheza na Chipolopolo ya Zambia bila mashabiki ugani Nyayo

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Francis Kimanzi ameridhishwa na ubora wa hali ya wanasoka wake wa Harambee Stars baada ya kuwaongoza kwa vipindi kadhaa vya mazoezi kwa minajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Chipolopolo ya Zambia mnamo Oktoba 9, 2020 ugani Nyayo, Nairobi.

Kimanzi pia amethibitisha kwamba kati ya wanasoka 23 wa mwisho aliowajumuisha kikosini, ni wawili pekee – Joseph Okumu anayechezea IF Elfsborg nchini Uswidi na Clarke Oduor anayesakatia Barnsley nchini Uingereza ndio hawajaripoti katika kambi yao ugani MISC Kasarani, Nairobi.

“Tuna kila sababu ya kusajili matokeo ya kuridhisha dhidi ya Zambia. Wachezaji wanaendelea kujitahidi mazoezini na viwango vya ushindani ni vya hali ya juu,” akasema mkufunzi huyo wa zamani wa Mathare United.

Mtazamo wa Kimanzi umeshadidiwa na beki Brian Mandela ambaye ameapa kujituma vilivyo na kuongoza Stars kutamba dhidi ya Zambia licha ya kwamba yeye ni miongoni mwa wanasoka ambao hawajashiriki mchuano wowote wa kimataifa katika kipindi cha miezi sita iliyopita.

Mchuano huo ambao awali ulikuwa uchezewe uwanjani MISC Kasarani sasa utatandazwa ugani Nyayo kuanzia saa kumi alasiri bila mashabiki. Kimanzi atategemea pakubwa wanasoka wa ligi mbalimbali za humu nchini katika mechi hiyo ambayo Stars wanatumia kujiandalia kwa mechi mbili za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2021 dhidi ya Comoros.

Mandela, ambaye amewahi kuwa nahodha msaidizi wa Stars, atalazimika kumudu ushindani mkali kutoka kwa mabeki Joash Onyango wa Simba SC (Tanzania) na Johnstone Omurwa wa Wazito FC.

Shirikisho la Soka Nchini (FKF) limewahakikishia Wakenya kwamba mechi kati ya Stars na Chipolopolo itapeperushwa moja kwa moja kupitia runinga ya StarTimes TV.

Kwa mujibu wa Nick Mwendwa ambaye ni Rais wa FKF, kupigwa marufuku kwa mashabiki kunatokana na maagizo ya Wizara ya Afya inayoendelea kudhibiti maambukizi zaidi ya ugonjwa wa Covid-19.

“Nashukuru Serikali imetukubalia kurejelea shughuli zetu, ingawa bila mashabiki uwanjani. Nafurahia soka imerejea na pia uwanja wa Nyayo upo katika hali nzuri ya kuandaa mechi za kimataifa baada ya miaka miaka mitatu ya ukarabati,” akasema Kimanzi.

Mwendwa alisema ingawa mashabiki 6,000 walikubaliwa kuhudhuria mashindano ya riadha majuzi uwanjani humo, soka ni tofauti kwa vile mashabiki wake ni tofuati kutokana na kushangilia kwao bao linapofungwa.

“Tunafuata maagizo ya Serikali huku tukitarajia mashabiki kukubaliwa katika mechi zijazo. Hii ni mechi ambayo Serikali itapania sana kutumia maafisa wa afya kutuchunguza ndipo iamue iwapo tunastahili kukubaliwa kuingia uwanjani kwa mara nyingine katika siku zijazo,” akaongeza Kimanzi ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya mabingwa mara 11 wa Ligi Kuu ya Kenya, Tusker FC.

KIKOSI CHA KENYA:

MAKIPA: Ian Otieno (Zesco United), Timothy Odhiambo (Ulinzi Stars);

MABEKI: Brian Mandela (hana klabu), Johnstone Omurwa (Wazito), Joash Onyango (Simba), Joseph Okumu (Elfsborg, Uswidi), Clarke Oduor (Barnsley, Uingereza), David Owino (Mathare United), Philemon Otieno (Gor Mahia), Badi Baraka (KCB);

VIUNGO: Kenneth Muguna (Gor), Francis Kahata (Simba, Tanzania), Cliff Nyakeya (Masr FC, Misri), Anthony Akumu (Kaizer Chiefs), Hassan Abdalla (Bandari), Lawrence Juma (Gor), Katana Mohammed (Isloch, Belarus), Austin Otieno (AFC Leopards);

WAVAMIZI: Elvis Rupia (AFC Leopards), Masoud Juma (JS Kabylie, Algeria), Timothy Otieno (Napsa Stars, Zambia), Oscar Wamalwa (Ulinzi Stars).

KIKOSI CHA ZAMBIA:

MAKIPA: Jackson Kakunta (Power Dynamos), Sebastian Mwange (Green Eagles) na Lameck Siame (Kabwe Warriors);

MABEKI: Kabaso Chongo, Tandi Mwape (wote kutoka TP Mazembe), Zachariah Chilongoshi, Kondwani Chiboni (wote wa Power Dynamos), Luka Banda (Napsa Stars), Dominic Chanda (Kabwe Warriors) na Benedict Chepeshi (Red Arrows);

VIUNGO: Kings Kangwa (Arsenal Tula, Urusi), Benson Sakala, Godfrey Ngwenya (Power Dynamos), Leonard Mulenga (Green Buffaloes), Kelvin Kapumbu (Zanaco), Amity Shamende, Gozon Mutale (wote Green Eagles), Edward Chilufya (Djurgardens IF, Uswidi), Lubambo Musonda (Slask Wroclaw, Poland), Kelvin Kampamba, Bruce Musakanya (wote Zesco United), Chaniza Zulu (Lumwana Radiants), Collins Sikombe (Napsa Stars);

WAVAMIZI: Evans Kangwa (Arsenal Tula, Urusi), Fashion Sakala (K.O Oostende, Ubelgiji), Gampahni Lungu (SuperSport United, Afrika Kusini), Emmanuel Chabula (Nkwazi) na Akakulubelwa Mwachiaba (Kabwe Warriors).

  • Tags

You can share this post!

Kamworor mkekani AK ikifichua kikosi cha Kenya kwa minajili...

Kipchoge ayoyomea Uholanzi kukutana na wasimamizi wake