Wakenya mawindoni ng’ambo kusaka mkwanja marathon mbalimbali
LILIAN Kasait na Isaiah Lasoi wanapigiwa upatu kufanya kweli Jumamosi watakapotimka Prague Half Marathon nchini Czech, katika wikendi yenye shughuli kibao za kutafuta donge nono na kuimarisha muda kwenye marathon na nusu-marathon mbalimbali.
Wawili hao wana muda bora kuliko wapinzani wao kwenye mbio hizo za kilomita 21 ambazo zimevutia washiriki 16,000. Lasoi anajivunia kukamilisha umbali huo kwa dakika 58 na sekunde 10. Wapinzani wake wakuu ni Wakenya wenzake Josphat Kiprotich (59:35) na Ezra Tanui (59:43).
Lasoi atamenyana pia na Wakenya wengine Josphat Kiprotich, Vincent Towett, James Kipkogei, Ezra Tanui, Moses Koech, Timothy Kipyego na Vincent Kiptoo.
Vile vile, watakuwepo Rodrigue Kwizera (Burundi), Faraja Lazaro (Tanzania) na Muingereza Joshua Adam huku Wakenya Michael Kirui, Luka Kurgat, Moses Cheruiyot na Henry Kiprono wakiwa wawekaji wa kasi.

Naye Kasait atapimwa vilivyo uwezo wake na Waethiopia Yalemget Mekuriyaw (saa 1:06:27) na Alemaddis Sisay (1:07:04).
Rekodi ya wanawake ya Prague Half inashikiliwa na Mkenya Joyciline Jepkosgei (saa 1:04:52). Muda huo ulimfanya kuwa mwanamke wa kwanza kukamilisha 21km chini ya saa 1:05:00.
Rekodi ya Prague Half ya wanaume iko mikononi mwa Sabastian Sawe (dakika 58:24). Rekodi hizo zinaweza kufutwa wikendi hii. Mshindi wa Prague Half atatia mfukoni Sh498,995, nao nambari mbili hadi sita Sh299,397, Sh199,598, Sh163,955, Sh121,184 na Sh71,285.
Nao Justus Kangogo, Asbel Rutto, Douglas Chebii, Stanley Kurgat, Charles Ndiema, Benard Kimeli, Bernard Muia, Mica Cheserek, Kipsambu Kimakal, Geoffrey Koech, Edward Koonyo, Evans Yego, Henry Kichana na Wisley Kibichii wako nchini Austria kwa mbio za Vienna Marathon hapo Jumapili. Mbio hizo zimevutia watu 45,000 wakiwemo 13,000 katika kitengo cha 42km.
Wakenya pia wanatarajiwa kutimka Berlin Half Marathon na Hannover Marathon nchini Ujerumani, Milan Marathon (Italia), Madrid Half Marathon (Uhispania) na Sao Paulo Marathon (Brazil).