• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:35 AM
Harlequins yaanza kujisuka upya kwa msimu ujao wa raga ya Kenya Cup

Harlequins yaanza kujisuka upya kwa msimu ujao wa raga ya Kenya Cup

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Kenya Harlequins kimemsajili aliyekuwa mwanaraga matata wa Homeboyz, Mark Wandetto kwa minajili ya kampeni za msimu ujao wa Ligi Kuu ya Kenya Cup.

Winga huyo alikuwa miongoni mwa wanaraga tegemeo katika timu ya taifa ya wachezaji saba kila upande, Shujaa, chini ya kocha wa zamani wa kikosi hicho, Paul Murunga.

Wandetto anajiunga na Quins siku chache baada ya kikosi hicho kujinasia pia maarifa ya Leroy Mbugua kutoka Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Anatazamiwa kuwajibishwa na Harlequins kwa mara ya kwanza katika kivumbi cha kitaifa cha Sevens Circuit mnamo Julai au Agosti 2020. Wandetto amekuwa mhimili wa Homeboyz kwa kipindi cha misimu miwili iliyopita.

Kwa mujibu wa Michael Wanjala ambaye ni mwenyekiti wa Quins, ujio wa Wandetto utakuwa kiini cha kufufuka kwa makali yao kadri kikosi chao kinavyojiandaa kujinyanyua katika msimu wa 2020-21 baada ya kuambulia nafasi ya tisa muhula huu.

“Tumeiwinda saini yake kwa kipindi kirefu. Analeta mwamko mpya kikosini, kasi na ubunifu mkubwa katika safu ya mbele,” akasema Wanjala kwa kusisitiza kwamba watapania pia kutegemea huduma za chipukizi wengi ambao wanatawaliwa na kiu ya kutambisha klabu katika kila pambano.

Quins wanajivunia idadi kubwa ya wanaraga chipukizi ambao wanalenga kuwakweza kutoka akademia hadi kikosi cha kwanza. Baadhi yao ni nahodha wa kikosi cha vijana wasiozidi umri wa miaka 20 Boniface Ochieng, Elisha Koronya na Melvin Thairu waliokuwa tegemeo kubwa la timu ya taifa ya wachezaji 15 kila upande, Simbas, mwaka jana.

Katika kivumbi cha msimu huu, Quins walisajili ushindi katika mechi tano na kupoteza jumla ya michuano 11 katika matokeo yaliyowashuhudia wakijizolea alama 28 pekee.

You can share this post!

Kanisa la PCEA lawapa chakula wahitaji wa msaada

Mfumaji matata wa Harambee Stars atangaza mipango yake mara...

adminleo