Hatima ya kipute cha Euro 2020 kuamuliwa hii leo Jumanne
Na MASHIRIKA
TURIN, Italia
SHIRIKISHO la Soka Italia (IFF) limetaka waandalizi wa Euro 2020 waahirishe kipute hicho ili kuwapa vinara wa soka nchini humo muda wa kutosha kufanikisha mikakati ya kukamilisha msimu wa Ligi Kuu ya Serie A, ambayo kwa sasa imesimamishwa kwa muda kufuatia mkurupuko wa virusi vya corona ulimwenguni.
Rais wa IFF, Gabriele Gravina amesema kwamba wazo hilo ni kati ya mambo muhimu yatakayowasilishwa kwa vinara wa Uefa leo katika kikao kitakachojumuisha wawakilishi na wajumbe wa mashirikisho yote 55 ya soka duniani.
Vinara wa Uefa watakongamana ili kuamua iwapo Euro 2020 itasitishwa kabisa, japo baadhi ya mataifa wanachama yametaka kipute hicho kuahirishwa hadi Disemba 2020 au mwanzoni mwa 2021.
Awali, mashindano hayo ya Euro yaliratibiwa kufanyika kati ya Juni 12-Julai 12 mwaka huu.
Japo uendeshaji wa mechi za Euro upo chini ya Uefa, huenda shirikisho hilo likalazimika kuzingatia agizo la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), ambalo limefutilia mbali mechi zote zilizoratibiwa kupigwa kati ya Machi na Aprili 2020 kutokana na hatari ya kusambaa zaidi kwa virusi vya corona.
Scotland walipangiwa kuwa wenyeji wa Israel katika nusu-fainali ya Machi 26 huku mshindi akilazimika kupimana ubabe na Norway au Serbia.
Wasimamizi wa Shirikisho la Soka la Norway (NFF) wamesisitiza kwamba hawatakuwa wenyeji wa mechi za nusu-fainali za kufuzu kwa Euro 2020, kutokana na kanuni zinazodhibiti kutengwa kwa wachezaji.
Isitoshe, timu za taifa za Ireland Kaskazini na Jamhuri ya Ireland, zilizokuwa zikutane na Bosnia-Herzegovina na Slovakia mtawalia, zimeomba mechi zao ziahirishwe na tarehe mpya kutolewa.
Mechi zote za kufuzu kwa Kombe la Dunia miongoni mwa mataifa ya bara Asia na Amerika Kusini pia zimeahirishwa.
Nayo michuano ya kirafiki dhidi ya Uingereza, Italia na Denmark baadaye mwezi huu sasa imefutiliwa mbali.
Kufikia sasa, mashindano yote ya soka nchini Uingereza yamesitishwa hadi Aprili 3 huku shughuli zote za michezo nchini Scotland, Italia, Uhispania, Ujerumani, Ufaransa, Uholanzi, Ureno na Amerika zikisitishwa.
Kwa upande wao, vinara wa FIFA pia wameomba vikosi mbalimbali kulegeza kanuni zinazodhibiti kuachiliwa kwa wachezaji wa mataifa mbalimbali katika kipindi cha miezi miwili ijayo.
“Tutawasilisha mapendekezo yetu kwa UEFA. Mipango yetu ni kuhakikisha Serie A msimu huu inakamilika. Haitakuwa haki kwa klabu iwapo msimu mzima utafutiliwa mbali,” akasema Gravina na kuongeza kuwa uwekezaji wa klabu katika Serie A hauchukuliwi vivi hivi.
Kwa mujibu wa gazeti la La Gazzetta dello Sport nchini Italia, IFF imependekeza kufanyika kwa michujo ili kuamua mshindi, kutokuwepo kwa mshindi wa Serie A katika msimu wa 2019-20 au mshindi kuamuliwa kwa kuzingatia msimamo wa sasa wa jedwali la Ligi Kuu.
Hata hivyo, Gravina anatumai kwamba kivumbi cha Serie A kitarejelewa na kutamatika rasmi kufikia Juni 30, mwezi mmoja baada ya tarehe ya awali iliyoratibiwa.
Mnamo Jumapili, Italia iliripoti vifo 368 kutokana na virusi vya corona, hii ikiwa rekodi ya idadi kubwa zaidi kushuhudiwa kwa siku moja tangu janga hili lianze.