Michezo

Hatutaki kulegeza kamba – Kibera Saints

December 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

MAKABILIANO makali yanazidi kutikisa kwenye mechi za kuwania taji la Nairobi West Regional League (NWRL) msimu huu.

Timu ya Kibera Saints ni kati ya vikosi vinavyopania kupambana mwanzo mwisho kutafuta tiketi ya kufuzu kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Pili muhula ujao.

”Hatutaki kulegeza kamba kwenye michuano ya msimu huu ambapo tumepania kutembeza gozi safi dhidi ya wapinzani wetu kuhakikisha tunafaulu kujikatia tiketi ya kusonga mbele,” kocha wa Saints, William Mulatya anasema na kuongeza kuwa hakuna lisilowekezana.

Anasema tayari wachezaji wake wameiva kupambana kwenye michuano ya Ligi za hadhi ya juu baada ya kupiga soka la viwango vya chini kwa zaidi ya miaka mitatu.

Kibera inaorodheshwa kati ya timu 21 zinazotazamiwa kushusha vita vya kibabe kwenye mechi hizo kutafuta tiketi ya kufuzu kupiga hatua msimu ujao.

”Katika mpango mzima muhula huu kauli mbiu yetu ni ‘This is our season’ maana tunahisi tunaweza.Tunaamini raundi hii hali haitakuwa kama ilivyotukuta msimu uliyopita maana licha ya kuanza mechi zetu vizuri baadaye tuliteleza na kumaliza pabaya,” kocha huyo alisema.

Anadokeza kuwa wanataka tiketi ya kusonga mbele wakilenga kufuzu kushiriki Ligi Kuu ya KPL ndani ya miaka mitatu au minne ijayo.

Saints inapatikana mtaani Kibera ambapo timu kadhaa kutoka eneo hilo zimeonyesha zinaweza baada ya kupiga hatua na kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Pili. Kocha huyo anaamini wachana nyavu wake wanatosha mboga pia wamekaa vizuri kupambana na wenzao katika mapambano ya Ligi za juu.

Kocha mkuu wake, Mark Tizodi anasema wanafahamu kampeni hizo kamwe hazitakuwa mteremko wala hakuna mpinzani wa kupuuza. ”Timu zote ni tisho kwa kila moja lakini WYSA na Maafande wa Nairobi Prisons zinakuja kwa kasi zaidi,” alisema na kuongeza kuwa ukizubaa tu utaachwa kwa mataa.

Kwenye juhudi za kujisuka kujiandalia kampeni hizo Saints ilitwaa huduma za vijana wanne wapya. Iliwaleta Boaz Owino na Mulana Muoka (Kibera Azzuri) pia Kevin Omondi (GORP FC) na Cyrus Koroma raia wa Liberia. Kadhalika itategemea huduma zake Enock Omosa aliyekuwa akichezea Uweza FC kwa mkopo msimu uliyopita.

Wengine ambao ndio wameunda Kibera Saints wakiwa: Collins Ochieng, David Omoro (nahodha), Briyan Obare, Brian Oduor Benson Wafula, Edwin Oduor, Moses Ochieng, Horrace Odem, Austin Ouma, Davis Ongangi, Seth Omondi, Brian Emori na Isaac Kimonyi.

Pia wapo Rhitzael Malobi, Kevin Kalani, Felix Ochieng, Enock Omosa, Kevin Omondi, Nickson Vidonyi, Isaiah Kativi, Cyrus Koroma na Fortune Lawrence.

Kwenye jedwali Saints chini ya nahodha, David Omoro inaongoza kwa kuzoa pointi 11, moja mbele KSG Ogopa baada ya kupiga mechi tano na nne mtawalia. WYSA ya tatu kwa alama tisa, moja mbele ya Nairobi Prisons nayo Uthiru Vision kwa alama sita inafunga nne bora.