Hatuwezi kujaza pengo la Manangoi, AK yasema
Na CHRIS ADUNGO
MWENYEKITI wa Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) Tawi la Nairobi, Barnabas Korir amesema haitawezekana kujaza pengo la mtimkaji Elijah Manangoi ambaye amejiondoa kwenye kikosi kitakachowakilisha Kenya katika Riadha za Dunia zitakazoandaliwa jijini Doha, Qatar kati ya Septemba 27 na Oktoba 6, 2019.
Manangoi ambaye alipigiwa upatu wa kutetea ufalme wa mbio za mita 1,500 jijini Doha alijiondoa kikosini mwanzoni mwa wiki hii kutokana na jeraha la goti ambalo limekuwa likimsumbua kwa muda.
Kulingana na Korir, AK haina uwezo wa kujaza nafasi ya Manangoi kwa kuwa alipata tiketi ya moja kwa moja ya kupeperusha bendera ya taifa nchini Qatar kutokana na ushindi uliomvunia nishani ya dhahabu katika Riadha za Dunia zilizoandaliwa jijini London, Uingereza mnamo 2017.
Wakati wa riadha hizo za 2017, Manangoi alimduwaza bingwa mara tatu wa dunia katika mbio za mita 1,500 Asbel Kiprop na kutia kapuni medali ya dhahabu baada ya muda wa dakika 3:33.61.
Ni ufanisi uliochangia Kenya iliyojizolea jumla ya nishani tano za dhahabu kukamilisha kivumbi hicho katika nafasi ya pili duniani nyuma ya Amerika.
Kaka mdogo
Kujiondoa kwa Manangoi, 26, kunasaza Kenya katika ulazima wa kuwategemea kwa sasa George Manangoi ambaye ni kaka mdogo wa Elijah, Ronald Kwemoi na bingwa mara tatu wa duru za IAAF Diamond League, Timothy Cheruiyot.
George na Cheruiyot ambaye aliambulia nafasi ya pili katika Riadha za Dunia za 2017, wamekuwa wakijinoa pamoja kwa kipindi kirefu hata kabla ya kikosi cha Kenya kinachojiandaa kuelekea Qatar kupiga kambi uwanjani MISC, Kasarani.