Michezo

HERI IKAE!: Manchester United wachoshwa na bei ya kunasa huduma za Maguire

June 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

BEKI Mwingereza Harry Maguire amekuwa akimezewa mate na Manchester City na Manchester United, lakini United sasa imejiondoa mbioni baada ya kuambiwa bei ya kunasa huduma zake ni rekodi ya dunia ya Sh12.9 bilioni.

United ilikuwa makini sana kunyakua beki huyu wa kati na kumfanya uti wa mgongo wa timu ya Ole Gunnar Solskjaer uwanjani Old Trafford.

Hata hivyo, mabingwa hao mara 20 walikuwa wameweka bei ya Maguire kuwa Sh7.7 bilioni na walipigwa na butwaa baada ya waajiri wake Leicester kuitisha Sh11.6 bilioni pamoja na nyongeza ya karibu Sh1.3 bilioni.

Maguire aligharimu ‘Foxes’ Sh2.2 bilioni alipojiunga nao kutoka Hull City mwaka 2017 na amejitokeza kuwa tegemeo wao.

Sasa, kila mtu anasubiri kusikia kama mabingwa Manchester City wako tayari kukubali bei hiyo ya Leicester inapotafuta kizibo cha Vincent Kompany. Kocha Pep Guardiola anaamini kwamba Maguire huenda akashirikiana vyema na Aymeric Laporte, ambaye amekuwa katika hali nzuri tangu atue uwanjani Etihad akitokea Athletic Bilbao miezi 18 iliyopita.

City imeonyesha iko tayari kutoa Sh8.4 bilioni kwa nyota huyu wa timu ya taifa ya Uingereza, ambaye amepata sifa tele katika kipindi kifupi cha miaka miwili pekee.

Hata hivyo, Leicester inashikilia kwamba itauuza kwa rekodi mpya ya dunia itakayofuta ile ya Sh9.7 bilioni inayoshikiliwa na Mholanzi Virgil van Dijk, ambaye alijiunga na Liverpool mwezi Januari mwaka 2018 kutokea Southampton.

Tetesi zinasema kwamba nahodha wa zamani wa Leicester, Matt Elliott anaamini kuwa mashabiki wa klabu hiyo wako tayari kumpa Maguire kwaheri bila pingamizi.

Mashabiki wakasirika

Mashabiki wa Leicester walionyesha hasira wakati klabu ziliweka ofa zikitafuta huduma za nyota kama Jamie Vardy, N’Golo Kante na Riyad Mahrez.

Hata hivyo, Elliott, 50, ambaye alichezea Leicester mechi 290 kati ya mwaka 1997 na 2004 anaamini mashabiki watakubali Maguire aondoke kwa bei nzuri bila kuhisi vibaya.

Aidha, Leicester pia ina mabeki Jonny Evans, Wes Morgan, Caglar Soyuncu na Filip Benkovic, 21, ambaye alikuwa Celtic kwa mkopo msimu uliopita. Elliott anaamini kocha Brendan Rodgers ataweza kukabiliana na maisha bila Maguire, ambaye amesakatia Uingereza mara 20.

“Napendezwa na mchezo wa Benkovic,” Elliot aliongeza. “Ana mwili mzuri wa mchezaji na huwa mtulivu akiwa na mpira. Amepata ujuzi Celtic na pia kutokana na kuchezea klabu tofauti katika mashindano ya Bara Ulaya.

“Tayari yeye ana ujuzi akiwa na umri mdogo. Sitashangazwa, bila ya kujali kama Maguire ataondoka, Benkovic akipata fursa kadhaa msimu ujao.”