• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
Higuain abanduka Juventus na kuyoyomea Amerika

Higuain abanduka Juventus na kuyoyomea Amerika

Na MASHIRIKA

FOWADI mkongwe raia wa Argentina, Gonzalo Higuain ameondoka kambini mwa Juventus baada ya mkataba wake na miamba hao wa soka ya Italia kutamatishwa kwa maafikiano.

Sasa anatazamiwa kuingia katika sajili rasmi ya kikosi cha Inter Miami kinachomilikiwa na mwanasoka nguli David Beckham nchini Amerika.

Higuain, 32, alijiunga na Juventus mnamo Julai 2016 baada ya kubanduka kambini mwa Napoli ambao ni watani wa tangu jadi wa Juventus kwa kima cha Sh10.5 bilioni.

Uhamisho wake huo ndio uliokuwa wa tatu ghali zaidi kuwahi kufanyika wakati huo duniani.

Diego Alonso ambaye ni kocha wa Inter Miami amethibitisha kwamba kikosi chake “kipo katika hatua za mwisho za kurasimisha uhamisho wa Higuain” ambaye amefichua azma ya kustaafu akinogesha kivumbi cha Major League Soccer (MLS) nchini Amerika.

Wiki iliyopita, Higuain alilakiwa katika uwanja wa ndege wa Miami na bwanyenye Jorge Mas ambaye ni miongoni mwa wamiliki wanne wa kikosi cha Inter Miami. Beckham ni nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza.

Higuain ambaye pia amewahi kuchezea Real Madrid, alifungia Juventus jumla ya mabao 66 kutokana na mechi 149. Amewahi pia kusakatia AC Milan ya Italia na Chelsea ya Uingereza kwa mkopo ila akashindwa kuridhisha mashabiki na kufikia malengo ya waajiri wake.

Mnamo Agosti 2020, kocha mpya wa Juventus, Andrea Pirlo alisema kwamba Higuain hayuko katika mipango ya baadaye ya miamba hao wa Italia.

“Alikuwa bingwa wa kutandaza boli, mchezaji wa haiba na tegemeo letu. Lakini kipindi chake kimekwisha na hayuko katika mipango yetu ya siku za usoni,” akasema Pirlo ambaye pia ni mwanasoka wa zamani wa Juventus.

TAFSIRI: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Shule za kibinafsi zaomba msaada

Nairobi na Nakuru zavuna zaidi katika pendekezo jipya la...