Higuain apoteza penalti mechi yake ya kwanza Inter Miami
Na MASHIRIKA
FOWADI Gonzalo Higuain, 32, alipoteza mkwaju wa penalti katika mchuano wake wa kwanza ndani ya jezi za kikosi cha Inter Miami inayomilikiwa na mwanasoka wa zamani wa Manchester United, David Beckham.
Inter Miami walipokezwa kichapo cha 3-0 na Philadelphia Union katika mechi hiyo ya Major League Soccer (MLS) mnamo Septemba 27, 2020.
Higuain ambaye ni raia wa Argentina, aliingia katika sajili rasmi ya Inter Miami mnamo Septemba 18, 2020 baada ya mkataba wake kambini mwa Juventus ya Italia kutamatishwa.
Nyota huyo ambaye pia amewahi kuvalia jezi za Chelsea, alipaisha penalti aliyoaminiwa kuchanja katika dakika ya 77.
Mechi hiyo ilikamilika kwa hisia kali baada ya Higuain kuzua vurugu kwa kumsukuma beki Jakob Glesnes aliyesherehekea bao la Philadelphia mbele yake.
Ingawa hivyo, kocha wa Inter Miami, Diego Alonso alieleza kuridhishwa na mchango wa Higuain katika mechi hiyo na kusisitiza kwamba sogora huyo atayaweka kando maruerue ya kupoteza penalti na kuwatambisha vilivyo katika mechi zijazo.
Mabao ya Philadelphia yalifumwa wavuni kupitia kwa Anthony Fontana, Ilsinho na Brenden Aaronson.
Inter Miami kwa sasa wanashikilia nafasi ya 13 kwenye jedwali la MLS Tawi la Mashariki kwa alama sawa na DC United. Philadelphia wanakamata nafasi ya pili kwa alama mbili pekee nyuma ya viongozi wa jedwali, Columbus Crew.
Higuain, 32, alijiunga na Juventus mnamo Julai 2016 baada ya kubanduka kambini mwa Napoli ambao ni watani wa tangu jadi wa Juventus kwa kima cha Sh10.5 bilioni. Uhamisho wake huo ndio uliokuwa wa tatu ghali zaidi kuwahi kufanyika wakati huo duniani.
Higuain ambaye pia amewahi kuchezea Real Madrid, alifungia Juventus jumla ya mabao 66 kutokana na mechi 149. Amewahi pia kusakatia AC Milan ya Italia kwa mkopo ila akashindwa kuridhisha mashabiki na kufikia malengo ya waajiri wake.
Mnamo Agosti 2020, kocha mpya wa Juventus, Andrea Pirlo alisema kwamba Higuain hayuko katika mipango ya baadaye ya miamba hao wa Italia.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO