Michezo

Hit Squad wajiandaa kwa Olimpiki

November 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

TIMU ya taifa ya ndondi almaarufu ‘Hit Squad’ imeimarisha matayarisho yake kwa minajili ya raundi ya mwisho ya mashindano ya kufuzu kwa Olimpiki za Tokyo, Japan mnamo 2021.

Kocha Benjamin Musa amesema kwamba wakufunzi wanafuatilia maendeleo ya wanamasumbwi mbalimbali ili kuhakikisha kwamba wako katika hali shwari ya kupambana.

“Kwa sasa tunashiriki mazoezi makali ya viungo vya mwili. Pia tunawapa mabondia fursa za kuchapana wao kwa wao huku tukiwaelekeza ipasavyo kuhusu mbinu za kuwakabili wapinzani. Baada ya kipindi kifupi kijacho cha kujifua, tutawapa wanariadha nafasi za kudhihirisha kiwango cha kuimarika kwao ulingoni,” akasema Musa.

Muda tayari ameridhishwa na kiwango cha ubora wa mabondia wake hasa ikizingatiwa kwamba wengi wao hawajawahi kushiriki mapambano yoyote tangu warejee nchini mwishoni mwa kivumbi cha bara la Afrika cha kufuzu kwa Olimpiki kilichoandaliwa jijini Dakar, Senegal mnamo Februari 2020.

Kabla ya kushuka ulingoni kwa kivumbi cha mwisho cha dunia cha kufuzu kwa Olimpiki, wanamasumbwi wa Hit Squad watapimana ubabe na wanandondi wa haiba kubwa katika kipute cha Mabingwa wa Mabingwa kitakachoandaliwa nchini Tanzania.

Kufikia sasa, ni mabondia Nick Okoth na Christine Ongare pekee ambao wamejikatia tiketi za kuwakilisha Kenya kwenye Olimpiki za Tokyo zitakazoandaliwa nchini Japan mnamo Julai 2021 baada ya kuahirishwa mwaka huu wa 2020 kwa sababu ya janga la corona.

Wawili hao ambao ni miongoni mwa wanamasumbwi 33 watakaowakilisha Afrika, walifuzu baada ya kutawala vitengo vyao kwenye mapambano ya Afrika ya kufuzu jijini Dakar.

“Tungependa kupata idadi kubwa zaidi ya wanamasumbwi ambao watafuzu kwa Olimpiki zijazo,” akasema Musa.

Kwa mujibu wa ratiba mpya ya mashindano hayo, michuano ya kufuzu kwa Olimpiki miongoni mwa mataifa ya bara Ulaya itaandaliwa kati ya Aprili na Mei 2021 huku ile inayojumuisha nchi za Amerika ikifanyika Mei 2021.

Kabla ya kusitishwa kwa shughuli zote za michezo duniani mnamo Machi 2020 kwa sababu ya janga la corona, jumla ya mabondia 16 wa vitengo vya flyweight na featherweight walikuwa wamejikatia tiketi za kunogesha Olimpiki za Tokyo.

Mnamo 2019, Kamati ya Kimataifa ya Ndondi za Olimpiki (BTF) ilitwaa usimamizi wa mechi zote za kufuzu kwa michezo hiyo katika jumla ya mabara matano.