Michezo

Hofu EPL klabu zikiripoti visa viwili vya Covid-19 mazoezini

May 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

VISA viwili zaidi vya maambukizi mapya ya virusi vya corona vimeripotiwa na klabu mbili tofauti katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Hii ni baada ya maafisa na wachezaji wote waliorejea kambini kwa minajili ya kampeni zilizosalia muhula huu kufanyiwa vipimo kati ya Jumanne na Ijumaa wiki ijayo.

Jumla ya watu 996 walifanyiwa vipimo hivyo na waliopatikana na virusi vya ugonjwa wa Covid-19 watatengwa kwa jumla ya siku saba.

Mwanzoni mwa wiki hii, kila klabu kati ya 20 zinazoshiriki kipute cha EPL ilitakiwa kufanya vipimo 50 kwa siku badala ya 40 vilivyopendekezwa awali.

Mnamo Mei 19, 2020, EPL ilifichua kwamba jumla ya maafisa na wachezaji sita wa ligi hiyo walipatikana na virusi vya corona baada ya watu 748 kufanyiwa vipimo vya afya.

Kati ya waliopatikana na virusi hivyo ni sogora Adrian Mariappa wa Watford na kocha msaidizi wa Burnley, Ian Woan.

Wanasoka wa EPL walianza mazoezi ya pamoja katika vikundi vya watu watano mnamo Jumanne iliyopita kwa mara ya kwanza tangu kivumbi hicho kuahirishwa mnamo Machi 13, 2020 kutokana na janga la corona huku zikiwa zimesalia mechi 92 zaidi.

Kampeni za EPL zimeratibiwa kuanza upya mnamo Juni 12, 2020 japo baadhi ya klabu na wachezaji wakiwemo N’Golo Kante (Chelsea), Troy Deeney (Watford), Danny Rose (Newcastle United) na Sergio Aguero (Manchester City) wamepinga vikali hatua hiyo.

Miongoni mwa vikosi ambavyo vimekuwa vikipinga maamuzi ya kurejelewa kwa EPL kabla ya corona kudhibitiwa vilivyo kote duniani ni Brighton, Watford na Aston Villa ambavyo kwa wakati fulani, vilitishia kujiondoa kwenye kampeni zilizosalia msimu huu.

Norwich ambao walipima maafisa na wachezaji wao mnamo Jumamosi, wanatarajiwa kuweka wazi matokeo yao hii leo Jumapili.

“Tunatoa habari hizi za jumla kwa minajili ya uwazi na uwajibikaji wakati huu ambapo shughuli za soka zinatarajiwa kurejea. Hakuna maelezo ya ziada yatakayotolewa kwa umma yakilenga vikosi vilivyoathiriwa wala wachezaji waliopatikana na virusi baada ya vipimo,” ikasema sehemu ya taarifa ya EPL.

Katika mkutano wa Mei 18, 2020, wachezaji walikubaliwa kurejelea mazoezi katika makundi ya watu watano. Hakuna kipindi chochote cha mazoezi kilichotakiwa kuzidi dakika 75.

Wachezaji na maafisa wa klabu zote 20 za EPL watakuwa wakifanyiwa vipimo vya afya kila baada ya saa 24 ili kubaini iwapo wana virusi vya corona au la.