• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:07 PM
Huenda Lallana akayoyomea Brighton

Huenda Lallana akayoyomea Brighton

Na CHRIS ADUNGO

BRIGHTON almaarufu ‘The Seagulls’ wako pua na mdomo kukamilisha usajili wa kiungo Adam Lallana kutoka Liverpool bila ada yoyote.

Mkataba wa Lallana na Liverpool unatamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu na nyota huyo amekuwa katika mazungumzo na Brighton kuhusu uwezekano wa kutua uwanjani American Express kwa kandarasi ya miaka mitatu.

Lallana, 32, amewasakatia Liverpool jumla 22 katika kampeni za msimu huu wa 2019-20 japo amepangwa katika kikosi cha kwanza katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mara tatu pekee.

Mara yake ya mwisho kuvalia jezi za timu ya taifa ya Uingereza ambayo imemwajibisha mara 34 ni katika mechi iliyowakutanisha na Italia mnamo Machi 2018.

Liverpool walimsajili Lallana kutoka Southampton mnamo Julai 2014 kwa kima cha Sh3.5 bilioni. Katika kipindi hicho cha miaka sita uwanjani Anfield, amesaidia Liverpool kunyanyua taji moja la EPL, moja la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Kombe la Dunia la Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) na ufalme wa Uefa Super Cup.

Kusajiliwa kwa Lallana kulifanikishwa na kocha Brendan Rodgers ambaye kwa sasa anayahemea pia maarifa yake kambini mwa Leicester City.

Wepesi wa Lallana wa kupata majeraha mabaya umemvurugia misimu yake kambini mwa Liverpool ambao amewachezea jumla ya mechi 16 ambazo zimemshuhudia akifunga bao moja pekee hadi sasa.

Wakati uo huo, kipa Ben Foster ametia saini mkataba mpya wa miaka miwili ambao kwa sasa utamdumisha kambini mwa Watford hadi atakapofikia umri wa miaka 39.

Mlinda-lango huyo alivalia jezi za Watford kwa mara ya kwanza mnamo 2005 akihudumia kikosi hicho kwa mkopo kutoka Manchester United. Tangu wakati huo, amechezeshwa mara 155 katika kipindi cha misimu miwili.

Nyota huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza amewajibishwa katika mechi zote za hadi kufikia sasa katika Ligi Kuu ya EPL msimu huu na akapangua jumla ya makombora 99.

  • Tags

You can share this post!

Pep alenga UEFA

Shinikizo mashabiki warejee uwanjani

adminleo