Huenda Liverpool watatawazwa wafalme katika uga tofauti
Na CHRIS ADUNGO
MECHI ambayo huenda ikashuhudia Liverpool wakitawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu itasakatiwa mbali na uwanja wao wa nyumbani wa Anfield.
Haya ni kwa mujibu wa maafisa wa usalama nchini Uingereza ambao kwa sasa wametaka vinara wa kipute hicho kuratibu upya michuano sita ya EPL ili kuepuka uwezekano wa kuzuka kwa ghasia, maandamano na vurugu miongoni mwa mashabiki.
Kati ya mechi ambazo zina historia ya kuwa kivutio kikubwa miongoni mwa mashabiki wa soka ya Uingereza ni gozi la Merseyside kati ya Liverpool na Everton na kivumbi ambacho huwakutanisha Manchester City na Liverpool.
Maafisa wa usalama wanapendekeza haja ya kuandaliwa kwa michuano hiyo, ambayo kihistoria hushuhudia mahudhurio ya idadi kubwa ya mashabiki, katika viwanja mbadala visivyo vya nyumbani kwa kikosi chochote.
Mpango huu, kwa mujibu wao, utazuia uwezekano wa baadhi ya mashabiki kushindwa kujizuia na kushawishika kukongamana nje ya viwanja husika vya timu za nyumbani kinyume na kanuni za afya zinazolenga kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.
Kipute cha EPL kinatazamiwa kurejelewa mnamo Juni 17 kwa mechi mbili zitakazokutanisha Aston Villa na Sheffield United kisha Manchester City na Arsenal.
Mechi hizo ni zile zilizokuwa zimesalia kwa vikosi hivyo kucheza ili kufikia idadi ya michuano 29 ambayo wapinzani wote wengine 16 walikuwa wamepiga hadi kipute hicho kiliposimamishwa kwa muda kutokana na janga la corona mnamo Machi 13, 2020.
Mechi zote za raundi nzima ya 30 zimeratibiwa kusakatwa kati ya Ijumaa ya Juni 19 na Jumapili ya Juni 21. Hadi kampeni za EPL zilipoahirishwa, zilikuwa zimesalia jumla ya mechi 92 za kutandazwa muhula huu.
Kipute cha EPL kitarejelewa siku 100 tangu Leicester City wawapokeze Aston Villa kichapo cha 4-0 mnamo Machi 9, 2020. Mechi zote zilizosalia zitasakatiwa ndani ya viwanja vitupu bila mahudhurio ya mashabiki.
Liverpool ambao wanafukuzia ufalme wa EPL kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 25 kuliko mabingwa watetezi Man-City wanaoshikilia nafasi ya pili huku zikiwa zimesalia raundi tisa zaidi za michuano.
MECHI AMBAZO HAZITASAKATIWA NYUMBANI KWA VIKOSI HIVI:
- Man-City na Liverpool
- Man-City na Newcastle
- Man-United na Sheffield United
- Newcastle na Liverpool
- Everton na Liverpool
- Mechi itakayoshuhudia Liverpool wakitawazwa mabingwa