Huenda Rais wa zamani wa IAAF akatupwa jela miaka 10
NA CHRIS ADUNGO
KESI ya aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF), Lamine Diack, imeanza jijini Paris, Ufaransa huku shutuma za ufisadi, utapeli na uvunjaji wa kanuni za uaminifu zikimwandama.
Waendeshaji wa mashtaka wa kesi hiyo wamedai kuwa Diack alipokea kima cha Sh415 milioni ili kuwaruhusu wanariadha wazawa wa Urusi waliotuhumiwa kutumia dawa haramu za kusisimua misuli (pufya) kuendelea kushiriki mashindano ya haiba kubwa yakiwemo yale ya Olimpiki za 2012 jijini London, Urusi.
Diack, 87, ameyakana madai hayo huku mawakili wake wakitaja tetesi hizo dhidi yake kuwa hazina msingi. Diack amekuwa akitumikia kifungo cha nyumbani nchini Ufaransa na yuko katika hatari ya kufungwa gerezani kwa kipindi cha miaka 10 iwapo atapatikana na hatia.
Mzaliwa huyo wa Senegal aliongoza IAAF kwa kipindi cha miaka 16 kati ya mwaka 1999 hadi 2015.
Rais huyo wa zamani wa IAAF anakabiliwa pia na masaibu ya kesi ya madai ya usafishaji wa fedha za ulaghai kwa kushirikiana na vinara mbalimbali wa riadha nchini Urusi kati ya 2000 na 2013.