Ian Baraclough ateuliwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Ireland ya Kaskazini
Na CHRIS ADUNGO
MWINGEREZA Ian Baraclough, 48, ameteuliwa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Ireland ya Kaskazini.
Haya ni kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Northern Ireland (IFA).
Baraclough amepokezwa mkataba wa miezi 18 utakaotamatika rasmi mwishoni mwa fainali za Kombe la Dunia zitakazoandaliwa nchini Qatar mnamo 2022.
Kocha huyo anajaza pengo la Michael O’Neill ambaye alimteua kuwa msaidizi wake katika kikosi cha chipukizi wasiozidi umri wa miaka 21 mnamo 2017.
Uteuzi wa Baraclough ulichochewa na ulazima wa kujaza pengo la O’Neill aliyeyoyomea Uingereza kudhibiti mikoba ya klabu ya Stoke City inayoshiriki Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship).
Baraclough ambaye ni beki wa zamani wa klabu ya Queens Park Rangers nchini Uingereza, aliaminiwa mikoba ya Northern Ireland baada ya kuibuka kidedea katika mahojiano yaliyojumuisha wakufunzi wengine wanne.
Kibarua chake kwa sasa ni kuwaongoza vijana wake kutamba katika mchujo wa Euro 2021, Nations League na fainali za Kombe la Dunia za 2022.
“Ni fahari tele kuteuliwa kudhibiti mikoba ya kikosi cha haiba kubwa kiasi hiki. Ni tija kubwa kunasibishwa na timu hii ambayo nitaiwajibikia kwa nguvu na uwezo wangu,” akasema Baraclough.
Mechi zake za kwanza ni mchujo wa Nations League utakaowakutanisha na Romania ugenini mnamo Septemba 4 kabla ya vijana wake kuwaalika Bosnia-Herzegovina kwa mchujo wa Euro mnamo Oktoba 8, 2020.
Baraclough anakuwa Mwingereza wa pili na kocha wa pili asiyekuwa mzawa wa Northern Ireland baada ya Lawrie McMenemy, kudhibiti mikoba ya kikosi hicho. McMenemy alikuwa mkufunzi wa Ireland Kaskazini kati ya 1998 na 1999.
Baraclough ndiye kocha anayejivunia ufanisi mkubwa zaidi katika kikosi cha U-21 cha Northern Ireland. Aliwahi kuongoza kikosi cha Sligo Rovers kutia kapuni ubingwa wa Ligi Kuu ya Ireland Kaskazini. Aliwahi pia kunyanyua mataji ya FAI Cuo na Setanta Cuo akidhibiti mikoba ya klabu hiyo mnamo Februari 2012.
Amewahi pia kudhibiti mikoba ya klabu za Motherwell, Oldham Athletic na Scunthorpe United nchini Uingereza.
Anajivunia kuwa kocha aliyewapokeza malezi ya soka masogora wa haiba kubwa kwa sasa kambini mwa Northern Ireland wakiwemo Bailey Peacock-Farrell, Jamal Lewis, Liam Donnelly, Jordan Thompson, Gavin Whyte na Mark Sykes.