Michezo

Ibrahimovic apona Covid-19

October 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

FOWADI mkongwe wa AC Milan, Zlatan Ibrahimovic amekamilisha kipindi chake cha karantini na amekubaliwa kurejea uwanjani kusakata kabumbu baada ya vipimo kuthibitisha kwamba amepona Covid-19.

Hayo ni kwa mujibu wa usimamizi wa AC Milan ambao wanashiriki Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Milan wametoa taarifa kusisitiza kwamba Ibrahimovic ambaye ni raia wa Uswidi, amefanyiwa vipimo viwili mfululizo vya corona na ikabainika kwamba amepona kabisa.

Kupitia mtandao wake wa Twitter, Ibrahimovic, 39, alisema: “Nimepona! Huu ni ushindi mkubwa dhidi ya Covid-19. Maafisa wa afya wamesema karantini imekamilika, kwamba sasa naweza kurejea uwanjani. Nitafanya hivyo kwa matao ya juu!”

Tangazo la kupona kwa Ibrahimovic linatolewa siku kadhaa baada ya Milan kutangaza kwamba sogora huyo alikuwa ameugua Covid-19 kwa mara ya pili mfululizo, tukio ambalo lingemweka nje ya gozi la Serie A kati ya Milan na Inter Milan mnamo Oktoba 17 uwanjani San Siro.

Ibrahimovic aliugua Covid-19 kwa mara ya kwanza mnamo Septemba 24, 2020.

Kwa mujibu wa vinara wa Serie A, huenda gozi la jiji la Milan likaahirishwa kwa kuwa wanasoka wawili wa AC Milan na watano wa Inter Milan bado wako karantini baada ya kupatikana na virusi vya corona.

Licha ya kukosa huduma za Ibrahimovic tangu Septemba 24, Milan bado wanajivunia mwanzo bora zaidi katika kampeni za Serie A msimu huu. Kikosi hicho kilipanda ngazi hadi kufikia nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Serie A baada ya kuibuka na ushindi katika mechi tatu za ufunguzi wa kampeni za Serie A muhula huu pamoja na kutinga hatua ya makundi ya Europa League.

Ili kujiandaa vilivyo kwa vipute hivyo vya haiba kubwa, AC Milan walimsajili beki raia wa Ureno, Diogo Dalot kutoka Manchester United kwa mkopo wa mwaka mmoja katika siku ya mwisho ya uhamisho wa wachezaji mnamo Oktoba 5, 2020.

Man-United waliweka mezani kima cha Sh2.6 bilioni mnamo Juni 2018 kwa minajili ya huduma za beki huyo mwenye umri wa miaka 21 kwa mkataba wa miaka mitano.

Mechi ya pekee ambayo Dalot alichezea Man-United msimu huu ni katika ushindi waliousajili dhidi ya Brighton kwenye gozi la EFL au Carabao Cup.

Ni kombora la Dalot ndilo lilichangia bao la pili lililofungwa na Marcus Rashford wa Man-United katika mechi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) iliyoshuhudia Paris Saint-Germain (PSG) wakibanduliwa mapema kwenye kivumbi hicho mnamo Machi 2019.

Man-United walipomsajili Dalot chini ya ukufunzi wa Jose Mourinho, wachanganuzi wa masuala ya soka ya Uingereza walimsifia pakubwa na kumtaja kuwa miongoni mwa mabeki chipukizi walio bora zaidi barani Ulaya.

Katika msimu wake wa kwanza kambini mwa Man-United, Dalot aliwajibishwa mara 23. Hata hivyo, alijipata katika ulazima wa kusugua benchi baada ya kusajiliwa kwa Aaron Wan-Bissaka. Dalot alichezeshwa na Man-United katika jumla ya michuano 11 pekee msimu uliopita wa 2019-20.