Michezo

Ibrahimovic atambisha AC Milan kwenye mchujo wa Europa League

September 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO 

BAO kutoka kwa mfumaji mkongwe Zlatan Ibrahimovic na jingine la kiungo Calhanoglu yalisaidia AC kucharaza kikosi cha Shamrock Rovers cha Ireland 2-0 jijini Dublin mnamo Septemba 17, 2020 kwenye mechi ya kufuzu kwa Europa League.

Ibrahimovic, 38, aliwaweka Milan kifua mbele kunako dakika ya 23 kabla ya kuchangia goli la pili lililojazwa wavuni na Calhanoglu katika dakika ya 67.

Nusura Ibrahimovic afungie waajiri wake bao la tatu mwishoni mwa kipindi cha pili. Hata hivyo, kombora lake lilibusu mwamba wa goli kabla ya kipa Gianluigi Donnarumma kufanya kazi ya ziada na kumnyima fowadi Aaron Greene nafasi mbili za wazi uwanjani Tallaght.

Ushindi wa Milan ambao ni mabingwa mara 18 wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A), unatazamiwa sasa kuwapa motisha zaidi ya kutamba zaidi katika mapambano mbalimbali ya soka msimu huu wa 2020-21.

Milan walikosa fursa ya kusakata soka ya bara Ulaya msimu uliopita baada ya kupigwa marufuku ya mwaka mmoja kwa hatia ya kuvunja kanuni za Uefa kuhusu matumizi ya fedha (FFP).

Mabingwa hao mara saba wa European Cup waliambulia nafasi ya sita kwenye Serie A msimu uliopita chini ya kocha Stefano Pioli.

Baada ya kukwaruza Shamrock, Milan kwa sasa wanatazamiwa kuvaana na Bodo Glimt ya Norway kwenye raudi ya tatu ya kufuzu kwa kivumbi cha Europa League msimu huu.

Shamrock ndicho kikosi cha kwanza cha Ireland kuwahi kutinga hatua ya makundi ya Europa League mnamo 2011. Kubanduliwa kwao na Milan kunawapa sasa fursa ya kumakinikia Ligi Kuu ya ambayo kwa sasa wanaiongoza kwa alama nane zaidi kuliko Bohemians wanaoshikilia nafasi ya pili.

Miamba hao wa soka ya Ireland waliaga tena kivumbi cha Europa League katika raundi ya pili ya mchujo baada ya kutandikwa jumla ya mabao 4-3 na Apollon ya Cyprus kwenye mechi za mikondo miwili.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO