Michezo

Icardi avuliwa unahodha huku Real Madrid ikimmezea mate

February 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA CECIL ODONGO

UONGOZI wa Inter Milan ya Italia umempokonya unahodha Mauro Icardi baada ya habari kuhusu kuhama kwa mshambilizi huyo hadi Real Madrid kuendelea kushamiri wakati mazungumzo ya kuomwongezea mkataba ukidaiwa kusambaratika..

Mnyakaji wa Inter Samir Handanovic sasa atakuwa kapteni mpya wa wapambe hao wa zamani wa Ligi Kuu nchini Italia(SerieA) na Klabu Bingwa Barani Uropa.

Agenti wa Icardi ambaye pia ni mkewe Wanda Nara hata hivyo amekuwa akisisitiza kwamba mumewe hana nia ya kuguria Uhispania ingawa amekuwa akiitaka Inter kumwongezea Mwaajentina huyo ujira ili awe akipokea mshahara unaowiana na hadhi yake kikosini.

Ingawa hivyo, Nara amekiri kwamba mumewe amekuwa akiwindwa na timu tajika zinazoshiriki ligi za hadhi nchini Uhispania, Ufaransa, Ujerumani na hata Uingereza.

Icardi, 25 amekuwa mhimili mkubwa kwa Inter baada ya kufunga mabao tisa katika mechi 20 za Serie A msimu huu wa 2019/20. Mrithi wake, Handanovic ataanza majukumu yake mapya Alhamisi Februari 14 katika mechi ya ligi ya Uropa ugani San Siro.

Mshambulizi huyo hata hivyo ana mktaba na Inter hadi mwaka wa 2021 lakini hatua ya uongozi wa timu kumpokonya ukapteni huenda inaashiria kwamba washakata tamaa kumzuia kutua Santiago Bernabeau.

Kikosi cha kocha Luciano Spalletti baada ya kushiriki mechi 23 za Serie A kinashikilia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la ligi hiyo nyuma ya viongozi Juventus na nambari mbili Napoli.

Tumaini la pekee la Inter kushinda taji hata hivyo lipo katika kipute cha ligi ya Uropa wanakotarajiwa kuilemea Rapid Vienna ya Austria kisha kutinga awamu ya robo fainali. Iwapo hilo halitatimia basi watakosa kutwaa taji lolote kufikia mwisho wa msimu huu.