Ighalo kuendelea kuwa 'Shetani Mwekundu' kwa miezi 7 zaidi
Na CHRIS ADUNGO
FOWADI Odion Ighalo amerefusha muda wake wa kuhudumu kambini mwa Manchester United kwa kipindi miezi saba zaidi hadi Januari 2021.
Ighalo, 30, alijiunga na Man-United mnamo Januari 2020 kutoka Shanghai Shenhua inayoshiriki Ligi Kuu ya China. Mkataba wake ulikuwa utamatike rasmi mnamo Mei 31, 2020. Kuongezwa kwa kandarasi ya sogora huyo mzawa wa Nigeria ugani Old Trafford kulichochewa na tukio la kusitishwa kwa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Machi 13 kutokana na janga la corona.
Hapakuwapo na kipengele kinachoruhusu Man-United kumpokeza Ighalo mkataba wa kudumu kwenye maagano yao ya Shenhua.
“Imekuwa tija na fahari kubwa kwake kwa sababu hiki kimekuwa kikosi ambacho amekuwa akikishabikia tangu utotoni. Ni matumaini ya kila mmoja kwamba atakamilisha alichokianzisha ugani Trafford na kushindia Man-United angalau taji moja muhula huu,” akatanguliza kocha Ole Gunnar Solskjaer.
“Shenhua wametufanyia hisani kubwa kwa kumkubalia Ighalo kuendelea kuvalia jezi za Man-United licha ya kwamba nao wanazihitaji huduma zake kwa sasa
Hadi kufikia sasa, Ighalo amefungia Man-United jumla ya mabao manne katika mechi nane. Goli lake la mwisho lilikuwa katika ushindi wa 5-0 waliousajili dhidi ya LASK kwenye kivumbi cha Europa League mnamo Machi 12, 2020. Kivumbi hicho kilikuwa cha mwisho kwa Man-United kupiga kabla ya kampeni za msimu huu kuahirishwa kutokana na janga la corona.
Kipute cha EPL kinatazamiwa kurejelewa mnamo Juni 17. Hadi kiliposimamishwa zikiwa zimesalia raundi tisa zaidi za mechi za kutandazwa muhula huu, Man-United walikuwa katika nafasi ya tano kwa alama nne chini ya Chelsea wanaofunga orodha ya nne-bora.
Mbali na kufukuzia taji la Europa League na nafasi ya kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao, Man-United pia wamo katika robo-fainali za Kombe la FA ambapo wamepangiwa kuvaana na Norwich City uwanjani Carrow Road.
Robo-fainali za mechi za kuwania ubingwa wa Kombe la FA msimu huu sasa zitaandaliwa wikendi ya Juni 27-28 huku fainali ikiratibiwa kutandazwa Jumamosi ya Agosti 1, 2020. Mechi za nusu-fainali za kipute hicho zitaskatwa kati ya Julai 18-19, 2020.
Droo ya robo-fainali za Kombe la FA ilifanyika mnamo Machi 9, 2020. Leicester City watakuwa wenyeji wa Chelsea ugani King Power, Manchester City wawaendee Newcastle United uwanjani St James’ Park nao Sheffield United wakwaruzane na Arsenal ugani Bramall Lane.