• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 3:55 PM
Imani tele fedha za bajeti zitainua vijana kispoti

Imani tele fedha za bajeti zitainua vijana kispoti

Na CHRIS ADUNGO

RAIS wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Nick Mwendwa amesema kiasi cha fedha ambacho sekta ya michezo ilitengewa katika bajeti ya kitaifa ya mwaka wa 2020-21 kitatosha kuimarisha makuzi ya michezo mbalimbali ya humu nchini.

Sekta ya michezo imetengewa Sh14 bilioni, hiki kikiwa ndicho kiwango kikubwa zaidi cha fedha kwa mara ya kwanza katika historia. Sekta hiyo ilipata nyongeza ya hadi asilimia 154 ya bajeti mpya kutoka mwaka wa kifedha wa 2019-20.

Mnamo 2019-20, Wizara ya Michezo, Sanaa na Utamaduni ilitengewa jumla ya Sh5.3 bilioni pekee kutoka hazina ya kitaifa. Hii inamaanisha kwamba ipo nyongeza ya Sh8.7 bilioni mwaka huu, fedha ambazo Mwendwa ameshikilia kuwa zitainua pakubwa mashirikisho mbalimbali ambayo tayari zimewasilisha bajeti zao kwa minajili ya kampeni za msimu ujao.

Mwingine ambaye amefichua matumaini yake kwamba fedha hizo zitaboresha maendeleo ya sekta ya michezo baada ya mashirikisho kuwezeshwa ipasavyo, ni Oduor Gangla ambaye ni Rais wa Shirikisho la Raga la Kenya (KRU).

“Fedha hizi zitaimarisha hali ya uchumi miongoni mwa vijana wetu ambao watapata nafasi nyingi za kazi kupitia michezo ya kila sampuli. Kwa kushiriki michezo hiyo hadi viwango vya kimataifa, watakuwa wakiletea Kenya fedha za kigeni na kutoa majukwaa mwafaka zaidi kwa maendeleo ya sekta nyinginezo, hususan utalii,” akatanguliza Waziri wa Fedha, Ukur Yatani.

Mwaka jana, FKF ndilo shirikisho lililopokea asilimia kubwa zaidi ya mgao wa fedha za Serikali huku likipata Sh252 milioni kwa minajili ya maandalizi ya fainali za Kombe la Afrika (AFCON) zilizofanyika nchini Misri.

FKF inatarajia pia kupokea kima cha Sh50 milioni kutokana na mgao wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA). Mwendwa amekariri kuwa asilimia kubwa ya fedha hizo itatengewa vikosi vya soka vinavyopitia hali ngumu zaidi ya kifedha.

Hatua hiyo itasaidia kuinua kiwango cha mapato ya klabu kadri zinazovyojitahidi kujikimu wakati huu wa janga la corona. Serikali tayari inatoa Sh10,000 kila mwezi kwa kila mchezaji wa vikosi 12 vya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) isipokuwa Bandari FC, Tusker, Posta Rangers, wanabenki wa KCB na wanajeshi wa Ulinzi Stars.

Fedha hizo ambazo ni mgao wa Sh20 milioni kutoka Hazina ya Kitaifa ya Michezo, zinanuia kuwapiga jeki baadhi ya wanaspoti ambao wamekuwa wakikabiliana na hali ngumu ya kimaisha baada ya michezo iliyokuwa kitega-uchumi kwao kusitishwa kwa sababu ya corona.

  • Tags

You can share this post!

Wito FKF ishauriane na timu za KPL

FKF kushtakiwa kwa kukosa kulipa Starlets

adminleo