Michezo

Ingwe kuchuana na Yanga kirafiki

August 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CECIL ODONGO

MABINGWA mara 13 wa Ligi Kuu (KPL) waliondoka nchini Ijumaa kuelekea taifa jirani la Tanzania kushiriki mechi ya kirafiki dhidi ya vigogo wa soka nchini humo Yanga SC, itakayokuwa Jumapili.

Mwenyekiti wa Ingwe, Dan Shikanda alithibitisha kuwa kikosi hicho kitagaragazana na wenyeji wao mjini Arusha, mechi ambayo watatumia kujifua kwa msimu mpya unaoanza mwezi Agosti 30.

“Kwa kweli tunasafiri kuelekea mji wa Arusha kuchuana na Yanga SC ambayo ni kati ya timu zenye historia pevu ya soka nchini bongo. Huu mchuano tuliupanga kama njia ya kunoa makali yetu kwa msimu unaoanza mwisho wa mwezi huu,” akasema Shikanda akizungumza na Taifa Leo.

Aidha alisema ziara hiyo nchini Tanzania itatumiwa na kocha Casa Mbungo kutesti wachezaji wapya na kuamua idadi ya wanasoka ambao wataunga na kukamilisha kikosi cha kwanza kwenye mechi za KPL msimu ujao.

Kocha huyo ambaye aliungana na Ingwe msimu jana, ana kibarua kigumu cha kuhakikisha ‘Chui’ wanarejelea ubora wao wa miaka ya zamani ili kutoa ushindani mkali kwa watani wao wa tangu jadi Gor Mahia ambao wametwaa ubingwa wa ligi mara 18.

Kama njia ya kujisuka kwa msimu mpya, AFC Leopards wamemsajili golikipa wa zamani wa Uganda Cranes, Benjamin Ochan na mlinzi matata Collins Shivachi kutoka kwa Tusker FC.

Caf

Yanga FC inayonolewa na Mwinyi Zahera, itatumia mechi hiyo ya kirafiki kujifua kwa mtanange mkali ya Klabu Bingwa Barani Afrika (Caf) dhidi ya Township Rollers ya Botswana ugenini wikendi ijayo.

Huku hatima ya udhamini wa Ligi Kuu bado ukiwa haujulikani, Shikanda aliwataka wafuasi wa AFC Leopards kujitokeza na kuisapoti timu hiyo kifedha, akisema msimu huu watawategemea mashabiki kugharamia malipo ya mishahara ya wachezaji na mambo mengine yanayohitaji fedha.

Afisa huyo pia alitoa wito kwa waliokuwa wapinzani wake kwenye uchaguzi uliopita wa maafisa wa timu kumuunga mkono ili kurejesha ufanisi kambini mwa Ingwe iliyoshinda KPL mara mwisho 1998.