Ingwe motoni baada ya mashabiki kumpiga refa
NA CECIL ODONGO
KLABU ya AFC Leopards imetakiwa kuyaweka hadharani majina ya mashabiki wake waliomwaangushia kipigo tosha msimamizi wa mechi kati yao na Nzoia Sugar Jumapili Januari 6, 2019 ugani Kenyatta, Machakos.
Rais wa Shirikisho la soka nchini(FKF) Nick Mwendwa ameapa kuichukulia hatua kali Ingwe ambao pia walikuwa mwenyeji wa mechi hiyo akisema vurugu na ukosefu wa maadili katika soka nchini ni suala ambalo limepitwa na wakati na halikubaliki kamwe.
“Tumewaamrisha AFC Leopards watuambie majina ya majangili waliompiga refa tena mchana peupe. Nimeshangazwa na tukio hilo kwasababu kwa muda tabia hiyo haijakuwa ikishuhudiwa katika ligi yetu. AFC Leopards ilikuwa timu ya nyumbani na wanafaa kutueleza waliohusika ni akina nani,” akasema Bw Mwendwa.
Mashabiki wa Ingwe walijitosa uwanjani baada ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi hiyo kupigwa na kumchapa refa wakilalamikia bao la dakika za jioni lililotiwa wavuni na Nzoia Sugar.
Refari huyo kwa jina George Mwai alivumilia kipigo hicho kwa muda kabla ya kuokolewa na maafisa wa usalama huku mashabiki hao wakisikika wakiapa kutomruhusu tena kusimamia mechi za timu yao.
Kikosi cha wachezaji 10 cha Nzoia kililazimisha sare ya 1-1 na AFC Leoapards na kuzidisha masaibu ya Ingwe ambao sasa wameshinda mechi moja tu msimu huu wa 2018/19