• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 3:09 PM
Ingwe yajitosa sokoni kusajili mastaa wa kuinyanyua kutoka eneo hatari ligini

Ingwe yajitosa sokoni kusajili mastaa wa kuinyanyua kutoka eneo hatari ligini

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa Kenya mara 13, AFC Leopards wamejitosa sokoni kwa kishindo kujisuka kwa mkondo wa lala-salama baada ya kunyakua David ‘Cheche’ Ochieng’ katika siku ya kwanza ya kipindi kifupi cha uhamisho mnamo Machi 11, 2019.

Beki huyu amesaini kandarasi ya muda mfupi. Kuwasili kwake ni habari njema kwa Leopards inayoshikilia nafasi ya 14 kwa alama 16 kutokana na mechi 16 kwenye ligi hii ya klabu 18. Ingwe pia ni moja ya klabu zinazovuja sana ligini baada ya kushuhudia nyavu zake zikitikiswa mara 22. Mount Kenya United ina rekodi mbaya zaidi ya kufungwa baada ya Leopards ikiruhusu magoli 33 kuingia katika nyavu zake.

Anatarajiwa kuanza kazi Ingwe itakapomenyana na mabingwa wa mwaka 2009 Sofapaka mjini Kakamega mnamo Machi 13, amecheza nje ya Kenya miaka sita kabla ya kurejea nyumbani.

Baada ya kuondoka Tusker FC mwezi Agosti mwaka 2013, alijiunga na Al-Taawon nchini Saudi Arabia kisha akaelekea New York Cosmos nchini Marekani mwezi Februari mwaka 2016 kabla ya kutua Brommapojkarna nchini Uswidi mwezi Januari mwaka 2018. Aliamua kuhama Brommapojkarna baada ya timu hiyo kumaliza Ligi Kuu katika nafasi ya 14 kati ya klabu zinazoshiriki ligi hiyo na kutemwa.

Cheche, 26, ambaye hajakuwa na klabu tangu aondoke Brommapojkarna mnamo Januari 1 mwaka 2019, ni mchezaji wa hivi punde kurejea katika ligi ya Kenya baada ya Dennis ‘The Menace’ Oliech. Mshambuliaji Oliech, 34, alijiunga na Gor Mahia mnamo Januari 2, 2019 kwa kandarasi ya miaka miwili. Oliech alikuwa amestaafu mwaka 2015 baada ya kusakata katika mataifa ya Qatar, Ufaransa na Milki za Kiarabu kabla ya kuajiriwa na Gor.

Kipindi hiki cha uhamisho kitafungwa Aprili 8, 2019.

  • Tags

You can share this post!

Mary Njoroge kusimamia mechi za AFCON U-17

Sarri amtetea Jorginho baada ya kuzomewa na mashabiki

adminleo