Michezo

Ingwe yapata kocha mpya kutoka Rwanda

February 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN ASHIHUNDU

AFC Leopards Jumatano ilimtangaza rasmi Andrew Mbungo Casa kama kocha wao mpya kujaza nafasi ya Marko Vasilijevic aliyejiuzulu mapema juma hili.

Akitangaza habari hizo jana, Katibu wa Leopards, Oscar Igaida alisema Mrwanda huyo mwenye umri wa miaka 52 amekubali mkataba wa mwaka mmoja unusu kuwanoa mabingwa hao wa zamani.

Baada ya kusaini mkataba huo, Mbungo alianza kazi mara moja baada ya kuwasili nchini mwishoni mwa wiki.

Mbungo alikuwa kwenye Ingwe ikicheza na Mount Kenya United mjini Machakos katika pambano la Ligi Kuu ya Kenya (KPL).

“Nimefurahia kujiunga na klabu hii ambayo ina wachezaji wengi wazuri. Nimefanya nao mazoezi na nimeridhika na uchezaji wao,” alisema Mbungo.

“Tatizo kuu hapa ni wachezaji kukosa Imani, ni kawaida timu yoyote kukosa Imani hasa baada ya kichapo cha 4-1 mikononi mwa Bandari, au kushindwa mara tatu mfululizo. Ni jukumu lango kuirejesha hiyo Imani huku tukilenga kupata matokeo mema katika mechi zijazo,” alisema.

“Tuliamua kumpa kazi baada ya kamati nzima ya uongozi kukubaliana. Nina hakika atadumisha nidhamu kikosini baada ya kuangalia rekodi yake ya taaluma,” aliongeza Igaida.

Mbali na klabu mbali mbali alizonoa, Mbungo aliweza kuiandaa timu ya taifa ya Rwanda kwa muda wa miezi sita.

Amesaidia klabu za AS Kigali na Kiyovu Sports kutwaa mataji ya kitaifa, vile vile ndiye aliyewaleta Jacques Tuyisenge na Francis Mustafa kujiunga na Gor Mahia pamoja na Soter Kayumba anayechezea Sofapaka.