• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 AM
Injera arejea kwenye Raga za Dunia baada ya kupuuza Shujaa kwa muda mrefu

Injera arejea kwenye Raga za Dunia baada ya kupuuza Shujaa kwa muda mrefu

Na GEOFFREY ANENE

MFUNGAJI wa zamani wa miguso mingi kwenye Raga za Dunia, Collins Injera yumo mbioni kuchezea Kenya baadaye mwezi huu katika mashindano haya baada ya kuwa nje mwaka mmoja na nusu.

Injera, ambaye mwaka 2016 jijini London nchini Uingereza alimpiku raia wa Argentina Santiago Gomez Cora na kuwa mfungaji wa miguso mingi kabla ya Mwingereza Dan Norton kumpita Aprili 2017, hakuchezea Kenya katika ligi hii ya mataifa 15 msimu 2018-2019 kutokana na mgomo.

Wachezaji wengi wazoefu akiwemo Injera walisusia kuwakilisha Kenya wakilalamikia mishahara yao kupunguzwa.

Kenya iliponea chupuchupu kutemwa kutoka mashindano haya ya duru 10 ambapo ilihitajika kufika robo-fainali katika duru ya mwisho jijini Paris nchini Ufaransa kukwepa kuangukiwa na shoka.

Injera alikosa duru mbili za kwanza za msimu huu wa 2019-2020 mjini Dubai (Milki za Kiarabu) na Cape Town (Afrika Kusini) mwezi Desemba mwaka 2019 baada ya kuumia akipeperusha bendera ya Kenya katika mashindano ya Safari Sevens jijini Nairobi mwezi Oktoba.

Kurejea kwake kumepokelewa kwa shangwe na Wakenya, hasa baada ya Jacob Ojee na Oscar Dennis kuumia. Hata hivyo, matarajio ya Wakenya kwake yatakuwa mengi, hasa baada ya Shujaa kuonyesha kuimarika bila yeye katika duru mbili za kwanza za msimu huu.

Licha ya kuambulia alama nne pekee mjini Dubai, vijana wa kocha Paul Feeney walitoa miamba Afrika Kusini na Uingereza kijasho chembamba katika mechi za malkundi. Shujaa itakutana tena na Afrika Kusini na Uingereza katika mechi za Kundi B za duru ya tatu mjini Hamilton nchini New Zealand mnamo Januari 25-26. Japan, ambayo inakamilisha orodha ya washiriki 16 baada ya kualikwa, iko pia katika kundi hili.

Shujaa itaondoka jijini Nairobi hapo kesho kuelekea New Zealand. Kikosi cha Shujaa: Andrew Amonde (nahodha), Jeffrey Oluoch, Alvin Otieno, Bush Mwale, Billy Odhiambo, Daniel Taabu, Collins Injera, Nelson Oyoo, Herman Humwa, William Ambaka, Johnstone Olindi, Vincent Onyala na Geoffrey Okwach.

You can share this post!

Fainali ya Chapa Dimba Mt Kenya kupigwa wikendi

Mahakama yazima uteuzi wa Wambui kusimamia uajiri

adminleo