• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
Inter Milan waaga kampeni za UEFA huku Shakhtar Donetsk wakishuka hadi Europa League

Inter Milan waaga kampeni za UEFA huku Shakhtar Donetsk wakishuka hadi Europa League

Na MASHIRIKA

INTER Milan walibanduliwa kwenye hatua ya makundi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa mara nyingine baada ya kulazimishiwa sare tasa na Shakhtar Donetsk ya Ukraine katika mechi ya Kundi B iliyochezewa uwanjani San Siro, Italia mnamo Disemba 9, 2020.

Hii ni mara ya tatu mfululizo kwa miamba hao wa soka ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kubanduliwa kwenye kivumbi hicho cha bara Ulaya.

Licha ya kutamalaki mchezo, kumiliki asilimia kubwa ya mpira na kubisha lango la wageni wao mara 20, bahati haikusimama na Inter Milan ambao walishuhudia fowadi wao Romelu Lukaku akipoteza nafasi nyingi za wazi.

Kipa wao Samiri Handanovic naye alilazimika kufanya kazi ya ziada ya kupangua makombora mazito aliyoelekezewa na wavamizi wa Shakhtar katika dakika za mwisho.

Matokeo hayo yalishuhudia Shakhtar walioambulia nafasi ya tatu kwa alama nane katika kampeni za Kundi B, wakishuka sasa kunogesha kampeni za Europa League.

Kundi hilo liliongozwa na Real Madrid kwa alama 10, mbili zaidi kuliko nambari mbili Borussia Monchengladbach ambao pia wamefuzu kwa hatua ya mwondoano. Chini ya mkufunzi Antonio Conte, Inter Milan walivuta mkia baada ya kujizolea alama sita pekee kutokana na mechi sita.

Shakhtar kutoka Ukraine, walipepeta Real katika michuano yote miwili iliyowakutanisha katika hatua ya makundi nyumbani na ugenini.

You can share this post!

DPP kukata rufaa dhidi ya kuachiliwa kwa bwanyenye Humphrey...

IEBC haitakagua saini za BBI bila ya kupewa pesa