Inter Milan wazamisha chombo cha Fiorentina katika dakika za mwisho-mwisho
Na MASHIRIKA
INTER Milan walifunga mabao mawili chini ya dakika tatu za mwisho wa kipindi cha pili na kuwachabanga Fiorentina 4-3 katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mnamo Septemba 26, 2020.
Christian Kouame aliwaweka wageni Fiorentina kifua mbele katika dakika ya tatu kabla ya Lautaro Martinez anayehusishwa pakubwa na Barcelona kusawazisha mwishoni mwa kipindi cha kwanza.
Federico Ceccherini alijifunga katika dakika ya 52 na kuwaweka Inter kifua mbele uwanjani San Siro kabla ya Gaetano Castrovilli na Federico Chiesa kufunga mabao ya haraka chini ya dakika sita na kuwarejesha Fiorentina uongozini.
Hata hivyo, Romelu Lukaku alisawazisha mambo katika dakika ya 87 kabla ya Danilo D’Ambrosio kukamilisha krosi ya Alexis Sanchez kwa kichwa na kuwapa Inter ya kocha Antonio Conte alama tatu muhimu.
Ilikuwa mara ya kwanza kwa mechi ya Serie A kushuhudia vikosi viwili vinavyomenyana vikibadilishana uongozi mara tatu tangu 2010 ambapo Inter waliwazamisha Siena hatimaye kwa mabao 4-3.
Conte, ambaye pia amewahi kuwanoa Chelsea, amesema kwamba kubwa zaidi katika maazimio yake muhula huu ni kunyima Juventus fursa ya kujinyanyulia taji la Serie A kwa msimu wa 10 mfululizo.