Ishara mfungaji bora EPL kuamuliwa siku ya mwisho msimu huu
Na CHRIS ADUNGO
VITA vya kuwania taji mfungaji bora katika soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu wa 2019-20 vinatarajiwa kuwa vikali zaidi katika jumla ya mechi saba zilizosalia kabla ya kampeni za kipute hicho kutamatika rasmi.
Mabao mawili yalifungwa na mshambuliaji Danny Ings katika ushindi wa 3-1 uliosajiliwa na Southampton dhidi ya Watford mnamo Juni 29 yalifikisha idadi yake ya magoli hadi 18, moja pekee nyuma ya Jamie Vardy wa Leicester City anayeongoza orodha ya wafungaji bora hadi kufikia sasa.
Kurejelewa kwa michuano ya EPL wikendi hii baada ya baadhi ya vikosi kupishwa kwa mapambano ya Kombe la FA kunatarajiwa kuwasha moto zaidi vita vya kusaka mshindi wa kiatu cha dhahabu.
Ikizingatiwa idadi ya mechi zilizosalia na mabao ambayo yanajivuniwa na wanasoka wanaopigiwa upatu kunyanyua taji hilo, dalili zote zinaashiria kwamba huenda mfungaji bora wa EPL msimu huu akaamuliwa katika siku ya mwisho.
Kufikia sasa, ni mabao sita pekee ndiyo yanatenganisha wanasoka 10 wa kwanza kwenye msimamo wa orodha ya wafungaji bora msimu huu.
WAFUNGAJI BORA WA EPL KUFIKIA SASA:
o Jamie Vardy (Leicester City) – 19
o Danny Ings (Southampton) -18
o Mohamed Salah (Liverpool) – 17
o Pierre-Emerick Aubameyang (Arsenal) – 17
o Sergio Aguero (Manchester City) – 16
o Sadio Mane (Liverpool) – 15
o Raul Jimenez (Wolves) – 15
o Marcus Rashford (Manchester United) – 14
o Anthony Martial (Manchester United) – 14
o Tammy Abraham (Chelsea) – 13
o Dominic Calvert-Lewin (Everton) – 13