Michezo

Ishara ya ‘ngono’ uwanjani yamletea noma Ronaldo nchini Saudi Arabia

March 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

CHRIS ADUNGO NA MASHIRIKA

SUPASTAA Cristiano Ronaldo amepigwa marufuku na kutozwa faini kwa kufanya kitendo kinachodaiwa kuwa cha kuudhi.

Nyota huyo wa zamani wa Manchester United na Real Madrid alifanya kitendo hicho cha kifidhuli wakati wa pambano kati ya Al-Nassr na Al-Shabab.

Ronaldo, 39, alisaidia waajiri wake kufunga Riyadh 3-2 mnamo Jumapili iliyopita katika gozi la Saudi Pro League.

Hata hivyo, kanda za video zilisambazwa mitandaoni zikimuonyesha akishika sikio lake la kushoto huku mkono wa kulia, aliouweka mbele ya fupanyonga, ukitoa ishara ya mtu anayeshiriki ngono. Ishara hiyo ilikuwa jibu la dharau kwa mashabiki wa Al-Shabab walioanza kuimba jina la Messi ambaye ni mtani mkubwa wa Ronaldo kitaaluma.

Sasa Kamati ya Nidhamu na Maadili ya Shirikisho la Soka la Saudi Arabia (SAFF) imetangaza kuwa Ronaldo atajutia matendo yake. Mbali na kukosa mechi ya Alhamisi kati ya Al-Nassr na Al-Hazm nyumbani, pia ameagizwa kulipa faini ya Sh779,340.

Pesa hizo zitaenda kwa klabu ya Al-Shabab ili kufidia gharama za klabu hiyo kuwasilisha malalamiko hayo rasmi. Ronaldo ametozwa pia nusu ya pesa hizo ambazo zitaendea SAFF ambayo imesisitiza kuwa Ronaldo hana fursa ya kukata rufaa.

Akijitetea, Ronaldo alisema ishara hiyo aliyoitia haikuwa ya matusi ila kusherehekea ushindi na imezoeleka sana katika soka ya bara Ulaya.

Si mara ya kwanza kwa Ronaldo kugonga vichwa vya habari kwa matendo yenye utata tangu ajiunge na Al-Nassr mnamo Januari 2023 baada ya kuagana na Man-United.

Mnamo Aprili mwaka jana, aliondoka ugani mwishoni mwa mechi dhidi ya Al-Hilal akiwa ameshika sehemu zake za siri. Tukio hilo lilichochea hasira za mashabiki walioanza kuimba tena jina la Messi.

Alidai wakati huo kwamba alikuwa akihisi maumivu kwenye sehemu zake za siri baada ya kuumia paja akiwa uwanjani.