Michezo

Itagharimu Arsenal Sh16b kumng’oa Isak kutoka Newcastle

June 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

LONDON, Uingereza

WANABUNDUKI wa Arsenal watalazimika kuvunja benki kupata huduma za mshambulizi matata Alexander Isak ambaye waajiri wake Newcastle United wametangaza bei yake kuwa zaidi ya Sh16.6 bilioni.

Timu hiyo kutoka jijini London, inatamani sana kupata raia huyo wa Uswidi mwenye asili ya Eritrea ili iimarishe makali yake katika kipindi cha uhamisho kinachofunguka Juni 14 hadi Septemba 2.

Inaaminika kuwa Arsenal wako tayari kumpa kocha Mikel Arteta fedha anazohitaji kuingia sokoni kwa mara nyingine wakilenga kupiga hatua moja mbele kwenye Ligi Kuu na kuvua Manchester City taji msimu ujao.

Kusajiliwa kwa Isak kunaaminika kunachukuliwa kwa uzito na kuwa Mswidi huyo anaenziwa sana ugani Emirates, ingawa Newcastle imesisitiza kuwa mshambulizi huyo hatauzwa.

Ripoti zinadai kuwa kitakachowafanya Newcastle wabadili msimamo ni iwapo zaidi ya Sh16.6 bilioni zitawekwa mezani.

Isak, ambaye aliwasili ugani St James’ Park kutoka Real Sociedad kwa Sh10.4 bilioni mwaka 2022, alifunga mabao 21 kwenye Ligi Kuu msimu 2023-2024 na bado anasalia na miaka minne katika kandarasi.

Mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 24 amekuwa akisisitiza kuwa anafurahia kuwa kambini mwa Newcastle na hajabadili msimamo.

“Nafurahia sana kuwa Newcastle,” Isak alisema katika mahojiano na tovuti ya Fotbollskanalen.

“Nilikuwa na msimu mzuri kabisa katika taaluma yangu. Huwezi kupuuza hilo. Napenda kila kitu kuhusu klabu hiyo, mashabiki, mji. Sina mawazo yoyote kuhusu kuondoka ama kitu kama hicho. Nafurahia kipindi changu na ninafurahia sana maisha yangu mle,” akasema Isak.

Mbali na Isak, Arsenal pia wanamezea mate Benjamin Sesko kutoka Leipzig nchini Ujerumani.

Ajenti wa Sesko alionekana majuzi akitazama mchuano kati ya Arsenal na Manchester United ugani Old Trafford mwezi Mei.

Chelsea pia wanaaminika kuvutiwa na Sesko, 21, na wamejaa imani kuwa wanaweza kushindana na ofa yoyote.