• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Italia sasa pua na mdomo kufuzu kwa fainali za Euro

Italia sasa pua na mdomo kufuzu kwa fainali za Euro

Na MASHIRIKA

TAMPERE, FINLAND

ITALIA sasa wanakaribia kufuzu kwa fainali za Euro 2020 baada ya penalti ya Jorginho kuwapa ushindi muhimu wa 2-1 dhidi ya Finland katika mchuano wa Kundi J uliowakutanisha mnamo Jumapili.

Jorginho ambaye ni kiungo wa Chelsea, alifunga penalti ya ushindi baada ya Sauli Vaisanen kuunawa mpira alioelekezewa na Nicolo Barella kunako dakika ya 78.

Awali, mvamizi Teemu Pukki wa Norwich City alikuwa amewasawazishia Finland kupitia penalti kunako dakika ya 72 na hivyo kuzifuta jitihada za Ciro Immobile aliyekuwa amewaweka Italia kifua mbele katika dakika ya 59.

Bao la Pukki lilikuwa lake la saba kutokana na jumla ya michuano sita ambayo amepiga hadi kufikia sasa msimu huu. Italia kwa sasa wanaongoza kundi lao kwa alama tisa zaidi kuliko Armenia ambao wanashikilia nafasi ya tatu. Italia kwa sasa wanahitaji alama nne pekee kutokana na mechi nne zijazo ili kujipa uhakika wa kunogesha fainali zijazo za Euro 2020. Italia kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Ugiriki na Lichtenstein mnamo Oktoba.

Immobile aliwafungulia Italia ukurasa wa mabao baada ya kushirikiana vilivyo na Federico Chiesa aliyempa krosi safi baada ya kupoteza nafasi kadhaa za wazi katika kipindi cha kwanza. Mchuo huo ulikuwa wa 10 kwa Chiesa kupiga bila ya kufunga bao tangu Septemba 2017 alipocheka na nyavu katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Isarel.

Pigo la pekee kwa Italia katika mchuano huo ni kuumia kwa beki Emerson ambaye kwa sasa atasalia mkekani wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) itakayowakutanisha Chelsea na Wolves mwishoni mwa wiki huu uwanjani Molineux.

Finland kwa sasa wanasalia katika nafasi ya pili kwenye Kundi J kwa alama tatu zaidi kuliko Armenia na hilo linawaweka pazuri zaidi kufuzu kwa fainali za Euro kwa mara ya kwanza katika historia. Timu zitakazoibuka katika nafasi mbili za kwanza zitafuzu kwa fainali za Euro 2020.

Kwingineko, Uhispania walikaribia kufuzu kwa Euro 2020 baada ya kuwapepeta Faroe Islands 4-0 katika Kundi F. Chini ya kocha Robert Moreno, ushindi huo uliwakweza hadi kileleni mwa kundi baada ya kutwala mechi zote sita zilizopita, hali inayowapa nafasi ya kujivunia alama saba zaidi kuliko Uswidi ambao ni wa pili.

Uswidi walilazimishiwa sare ya 1-1 na Norway baada ya bao la Stefan Johansen kufutiliwa mbali na Emil Forsberg mnamo Jumapili.

Mabao ya Uhispania yalifumwa wavuni na Rodrigo wa Valencia aliyefunga mawili kabla ya Paco Alcacer wa Borussia Dortmund kutikisa nyavu mara mbili mwishoni mwa kipindi cha pili.

Katika mchuano mwingine, Henrihk Mkhitaryan alifunga mabao mawili na kuchangia mengine mawili katika ushindi wa 4-2 uliosajiliwa na Armenia dhidi ya Bosnia-Herzegovina. Mkhitaryan kwa sasa anachezea Roma kwa mkopo wa msimu mmoja kutoka Arsenal.

Mabao ya Bosnia yalifungwa kupitia kwa Amer Gojak na Edin Dzeko. Ireland waliwalazimishia Denmark sare tasa katika mchuano mwingine wa Kundi D.

You can share this post!

Ranieri miongoni mwa wanaomezea ukocha Guinea

Harambee Stars yamiminiwa sifa kwa sare na UG

adminleo