• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
ITASALIA NDOTO: Neymar kuendelea kupiga soka nchini Ufaransa

ITASALIA NDOTO: Neymar kuendelea kupiga soka nchini Ufaransa

Na MASHIRIKA

PARIS, UFARANSA

NEYMAR atasalia kupiga soka yake ya kulipwa nchini Ufaransa msimu ujao baada ya Barcelona kukiri kwamba uwezo wao wa kifedha kwa sasa hautoshi kuwashawishi Paris Saint-Germain (PSG) kumwachilia fowadi huyu.

Yalikuwa matarajio ya Barcelona kuona mshambuliaji huyu mzawa wa Brazil akishirikiana tena na nyota Luis Suarez na Lionel Messi ugani Camp Nou huku ujio wa Antoine Griezmann ukiwafanya miamba hao wa Uhispania kuwa kikosi kinachojivunia wavamizi matata zaidi duniani.

Barcelona wamekuwa wakipania kumrejesha Neymar uwanjani Nou Camp, miaka miwili tu baada ya kumwachilia kujiunga na PSG kwa kima cha Sh26 bilioni.

Kufanikisha hilo, walitazamia kuwatia mnadani wachezaji wao Philippe Coutinho, Ivan Rakitic na Ousmane Dembele ili kupata kiasi cha fedha zilizotakiwa na PSG ili kumwachilia Neymar ambaye amekosa michuano yote ya kujifua kwa waajiri wake muhula huu.

Kwa mujibu wa gazeti la L’Equipe nchini Ufaransa, Neymar yuko radhi kususia kila kitu kambini mwa PSG ili apate idhini ya kurejea Barcelona ambao aliwachochea kunyanyua ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2015.

“Sitaki tena kuchezea PSG. Natamani sana kurudi Barcelona ambao kwa kweli, nisingekatiza uhusiano nao,” akasema Neymar mwishoni mwa mwezi jana.

Wepesi wa Neymar kupata majeraha mabaya ambayo humweka mkekani mara kwa mara ni suala ambalo limechangia sana kudidimika kwa ushawishi wake kambini mwa PSG.

Jeraha

Jeraha la goti alilopata mnamo Februari 2019 ni kiini cha kubanduliwa mapema kwa PSG kwenye kampeni za UEFA baada ya kuzidiwa maarifa na Manchester United waliotoka nyuma kwa mabao 2-0 na kuwapepeta katika mechi ya marudiano uwanjani Parc des Princes.

Neymar ambaye ni mchezaji ghali zaidi duniani, alipata jeraha la kifundo cha mguu mwezi jana wakati wa mchuano wa kirafiki uliowakutanisha Brazil na Qatar.

Jeraha hilo lilimkosesha fursa ya kushiriki fainali za Copa America zilizoandaliwa na Brazil ambao baadaye walitawazwa mabingwa baada ya kuwapepeta Peru.

Kwa pamoja na beki Presnel Kimpembe ambaye pia anauguza jeraha, Neymar hatakuwa sehemu ya kikosi cha PSG kitakachochuana leo na Sydney FC kirafiki mjini Suzhou, China.

Mwishoni mwa Juni, Barcelona walimpa Neymar masharti matatu ambayo alitakiwa kutimiza ili arejee upya ugani Camp Nou.

Zaidi ya kukubali mshahara mdogo kuliko ule wa hadi Sh56 milioni ambao kwa sasa anapokezwa na PSG kila wiki, pia alitakiwa kufutulia mbali kesi dhidi ya Barcelona kuhusu bonasi na marupurupu ambayo hakupokezwa wakati akivalia jezi za kikosi hicho.

Alitakiwa pia kukiri peupe kwamba ana nia ya kurejea Barcelona na aandike barua ya kushinikiza PSG kumwachilia.

  • Tags

You can share this post!

GUMZO LA SPOTI: Napoli yalima Liverpool huku Lyon...

VIDUBWASHA: Utaweza kujipima macho ukiwa nyumbani (The...

adminleo